Okwi, Bocco, Kichuya watikisa Simba

Muktasari:

Washambuliaji hao watatu wamekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Simba msimu huu katika Ligi Kuu Bara


Dar es Salaam. Mabosi wa Simba wajanja sana. Jamaa hao wana akili sana na kwa kuwa hawataki kupishana tena na taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara, wamewatengea fungu la maana nyota wake Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya ili kuwapa mzuka Bara.

Mabosi wa Simba wameamua kuwatengea nyota wake hao kiasi cha Sh100 milioni ili kuhakikisha wanaweka rekodi ya kuvunja mwiko wa kukaa kwa muda bila kubeba taji la Ligi Kuu Bara. Simba ina msimu wa tano sasa ihaijabeba ndoo ya VPL. Mara ya mwisho kubeba taji hilo ilikuwa msimu wa 2011-2012 wakati huo Jonas Mkude akiwa kinda ndani ya kikosi hicho akitokea kupandishwa timu ya Vijana U20.

Kama mnavyojua, Simba ndio kinara wa Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na alama 46 sawa na Yanga, ila uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa unaibeba mbali na mechi mbili mkononi dhidi ya moja ya watani zao wakati ligi ikiwa raundi ya 22.

Simba itaanza kula viporo vyake Aprili 3 kwa kuvaana na Njombe Mji kabla ya kusubiri kuvaana na Mtibwa Sugar ambao pia wana kiporo na Yanga.

Kutokana na kasi kubwa ya watani zao Yanga, Simba imeamua kufanya mambo yake kwa ustadi mkubwa ikiwemo kuweka mezani fungu hilo la fedha.

ISHU IPO HIVI

Kwa utaratibu wa Simba kila mechi wanayoshinda wachezaji hupewa Sh10 milioni kama posho ili wagawane na sasa uongozi wa timu hiyo umesisitiza Mil 100 ziko tayari na ni wachezaji tu kuamua kushinda mechi zilizosalia ili kubeba taji Msimbazi na pia kuvuna mkwanja huo.

Fedha hizo hutolewa mara tu baada ya wachezaji kushinda mechi na Meneja wa timu hiyo, Richard Robert ndiye huenda uwanjani na fungu hilo ili kuwamwagia nyota wa Msimbazi.

Kwa hesabu zilivyo ni; kwamba Nyota wa Msimbazi wamevuna kiasi cha Sh130 milioni mpaka sasa kwa kushinda mechi 13, hiyo ikiwa ni posho tu, achilia mbali mishahara na marupurupu mengine.

Wachezaji hao wamepoteza posho hizo kwenye mechi saba ambazo wametoka sare dhidi ya Azam, Yanga, Mtibwa Sugar, Stand United, Mwadui, Lipuli  na Mbao FC.

Hata hivyo kwa sasa wamepania kuweka fungu hilo mfukoni kwa kupeleka furaha ya ubingwa Msimbazi.

MSIKIE MANARA

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amesisitiza posho za wachezaji hao zipo na wanachopaswa kufanya ni kupambana tu ili waweze kushinda mechi zilizosalia.

"Tumekuwa tukitoa posho hizo za Sh10 milioni tangu msimu umeanza. Ni utaratibu wa kawaida kwenye timu yetu na wachezaji wote wanafahamu kuwa wakishinda mchezo mmoja wanaweza kupata kiasi gani cha fedha.

"Muhimu kwao ni kuendelea kujituma, posho zetu zitaendelea kuwa hizo mpaka msimu unamalizika na kama tutashinda mechi zote basi watavuna fedha nyingi zaidi," alisisitiza Manara.

Hata hivyo nyota hao wa Simba wanaweza kuvuna fedha zaidi kwani dau hilo la posho litapanda kwenye mechi dhidi ya Yanga kutokana na uzito wa mchezo wenyewe. Mara nyingi kwenye mechi dhidi ya Yanga nyota hao wamekuwa wakiwekewa kiasi cha Sh20-40 milioni ili kuwaongezea morali ya kushinda mechi.

Simba inahitaji kushinda dhidi ya Yanga ili kuongeza wigo wa pointi baina yao na kujiweka kwenye njia nzuri ya kutwaa taji hilo wakati huu ambao wapinzani wao Yanga wanakabiliwa na ukata mkubwa.

"Kwenye mechi kubwa kama dhidi ya Yanga na Azam huwa tunapandisha posho hizo kidogo kutokana na ugumu wa mechi. Kwenye michezo ya kawaida utaratibu unabaki ule ule," alisema Manara ambaye ni mtoto wa nguli wa zamani wa soka nchini, Sunday Manara.

KULA VIPORO MAPEMA

Simba tayari imepangiwa ratiba ya mechi zake mbili zinazofuata ambapo watacheza ugenini dhidi ya Njombe Mji Aprili 3 na kisha kukipiga na Mtibwa Sugar siku tano baadaye mkoani Morogoro.

Manara alisema kwa sasa wamejidhatiti kupata pointi hizo sita ugenini kwa kushinda mechi zote mbili na mipango yao ya ndani na nje ya uwanja iko vizuri.

"Lengo letu ni kutwaa ubingwa, kwa sasa tunaweka nguvu kubwa kwenye mechi zilizopo mbele yetu. Tumejidhatiti kushinda dhidi ya Njombe na kisha Mtibwa Sugar, baada ya hapo mipango ya michezo mingine itaendelea," alisema Manara.