Nyota wawili wawavuruga mabosi Mwadui FC

Muktasari:

  • Tayari Luhende ameshajiunga na Kagera Sugar, huku Nonga na Athuman wakiwa mikononi mwa Kocha Seleman Matola anayekinoa kikosi cha Lipuli kwa ajili ya msimu ujao.

MWANZA. MWADUI FC imesema kuwa kuondoka kwa nyota wao,David Luhende,Paul Nonga na Miraji Athuman ‘Sheva’ imewaachia pengo kubwa na kwamba kwa sasa wanaumiza vichwa ili kupata mbadala wao.
Tayari Luhende ameshajiunga na Kagera Sugar, huku Nonga na Athuman wakiwa mikononi mwa Kocha Seleman Matola anayekinoa kikosi cha Lipuli kwa ajili ya msimu ujao.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Ramadhan Kilao alisema kuwa kuondoka kwa wachezaji hao ni pigo kubwa kwani hawakutarajia kuwakosa nyota hao msimu ujao.
Alisema kuwa baada ya kuondoka kwao, kwa sasa uongozi unapambana kusaka wachezaji watakaoweza kuziba nafasi zao kwa ajili ya msimu ujao.
“Kuondoka kwa wachezaji hao kwa ujumla ni pengo kubwa kwetu,mchezaji kama Luhende hatukujua kabisa kama angeondoka lakini ndio maisha ya mpira tunajipanga kusaka mbadala wao,” alisema Kilao.
Kilao aliongeza kuwa malengo yao ni kuongeza wachezaji wanne katika nafasi ya Beki wa kushoto na Ushambuliaji pamoja na kujaza nafasi ya Kocha Msaidizi na kwamba mambo yanaenda vizuri.
“Mazungumzo kwa wachezaji na Kocha Msaidizi yanaendelea vizuri na muda wowote tutamalizana nao ili kuanza rasmi kazi,tumejipanga kufanya vizuri,” alisema Kilao.
Alisema kuwa hadi sasa timu inaendelea kujifua chini ya Kocha wao, Ally Bizimungu kwa wachezaji waliopo,huku akisubiri wengine wapya kwa ajili ya msimu ujao.