Nyota wa Man Utd wamkera Mourinho

Monday April 16 2018

 

London, England. Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho amesema wachezaji wake wanastahili adhabu baada ya kunyukwa na West Bromwich Albion.

Man United ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Old Trafford ilichapwa bao 1-0 na kupoteza ndoto ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Majirani zao Manchester City wametwaa ubingwa kutoka mikononi mwa Chelsea ikiwa na pointi 87 na Man United 71.

Mourinho alisema uzembe wa wachezaji kushindwa kufunga mabao ya mapema umewagharimu na walistahili kuchezea kichapo kutoka kwa wapinzani wao.

Bao pekee la dakika ya 73 lililofungwa na mshambuliaji Jay Rodrieguez lilimchefua Mourinho ambaye aliondoka uwanjani akiwa amefura kwa hasira.

Kocha huyo alidai baada ya ushindi wa kushangaza wa mabao 3-2 dhidi ya Man City, wachezaji walibweteka na kusahamu majukumu yao katika mechi zinazofuata.

“Baada ya ushindi dhidi ya Man City walijiona wako  juu ya mwezi na kusahau bado tulikuwa na kazi ngumu mbele yetu. Lakini sio wachezaji tu hata mashabiki walidhani kazi imemalizika,” alisema Mourinho.

Kocha huyo alidai katika kipindi cha wiki moja alifanya kazi ya ziada kuwajenga kisaikolojia wachezaji kujiandaa na mchezo dhidi ya West Bromwich inayoburuza mkia katika msimamo wa lgi ikiwa na pointi 24.

Mourinho alisema Man City inastahili kuwa mabingwa, lakini Man United ilikuwa na nafasi ya kuizuia kutangaza ubingwa mapema endapo mchezo wa jana ingeshinda.