Nyota wa Chelsea aliyekulia Tanzania

Muktasari:

  • Huenda mshambuliaji huyo ambaye alizaliwa Septemba 10, 1995 kwenye mji wa Kismaayo, Somalia angekuwa miongoni mwa mastaa wanaotamba Ligi Kuu Bara kama ilivyo kwa Shiza Kichuya wa Simba na Ibrahim Ajibu wa Yanga.

MAISHA yanaenda kasi sana. Miaka 18 iliyopita mshambuliaji wa Chelsea ya nchini England, Islam Feruz na wazazi wake Aisha ambaye ni mama na baba yake, Albashir Ali walikuwa wakiishi Tanzania kabla ya kutimkia zao Uingereza.

Huenda mshambuliaji huyo ambaye alizaliwa Septemba 10, 1995 kwenye mji wa Kismaayo, Somalia angekuwa miongoni mwa mastaa wanaotamba Ligi Kuu Bara kama ilivyo kwa Shiza Kichuya wa Simba na Ibrahim Ajibu wa Yanga.

Feruz mwenye umri wa miaka 22 amechukua uraia wa Scotland na sio Somalia wala Tanzania ambako amekulia kabla ya kwenda kuanza maisha yake ya soka nchini Scotland.

Historia inaonyesha Feruz alizaliwa Somalia na mwishoni mwa miaka ya 90 familia yake ikahamia Tanzania ambapo ilikaa kwa miaka kadhaa na baadaye mshambuliaji huyo alipofikisha miaka mitano ikahamia jijini London, England.

Mara baada ya kutua England, nyota huyo alijipatia elimu ya kawaida kwenye shule ya Hillhead iliyopo Glasgow, Scotland karibu na Chuo Kikuu cha Glasgow.

Akiwa na miaka 10, Feruz kipaji chake cha kucheza soka kilivumbuliwa na John Simpson ambaye alikuwa ni kocha wa vijana wa Celtic wakati huo alikuwa akiichezea Kickabout kwenye Kituo cha Michezo cha Castlemilk kama kilivyo kile cha Jakaya Kikwete Youth Park kilichopo Jijini Dar es Salaam.

Simpson alimchukua Feruz na kumuunga na akademi ya Celtic chini ya miaka 14 wakati huo yeye alikuwa na miaka 11. Kocha aliyekuwa anakinoa kikosi hicho, John Sludden alisema dakika 20 zimetosha kueleza kuwa nyota huyo aliyekulia Tanzania ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu.

Kocha huyo alikwenda mbali zaidi na kumfananisha Feruz na nyota wengine waliofanya makubwa, Paul McStay, Charlie Nicholas na Aiden McGeady. Alipofikisha miaka 12, familia yake alifukuzwa nchini humo na ilitakiwa kurejea Afrika.

Chaguo kwa familia hiyo ilikuwa ni kurejea Tanzania, lakini kocha mwingine wa vijana wa Celtic, Tommy Burns aliipigania familia hiyo kutokana na uwezo aliokuwa nao Feruz kutimuliwa kwao kulibatilishwa na wakatoa urai kwa kijana huyo.

Feruz alicheza mchezo wake wa kwanza akiwa na Celtic, 2009 ambapo alikuwa na miaka 14, mshambuliaji huyo alibaki kwenye kumbukumbu za kocha wake Tommy Burns kutoka na makubwa ambayo alikuwa akiyafanya.

Januari 14, 2011 Manchester City ilitajwa kumuwania mshambuliaji huyo ambaye alinaswa na Chelsea huku akiacha simanzi kwa kocha wa Celtic, Neil Lennon ambaye alimtupia lawama wakala wake kwa kusema alimshauri vibaya kinda huyo.

Septemba 2011, baada ya kuondoka Celtic ambako alikataa kusaini mkataba wake wa kwanza wa kuanza kucheza soka la kulipwa, alisajiliwa kwa mkataba uliotajwa kuwa na thamani ya Paundi 2,500 kwa wiki.

Feruz alikichezea kikosi cha kwanza cha Chelsea kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya mastaa wa ligi ya Malaysia, Julai 21 2013, aliingia dakika ya 32 kuchukua nafasi ya kiungo Kevin De Bruyne, lakini mapumziko alitolewa na nafasi yake akaingia André Schürrle.

Mshambuliaji huyo ambaye amekulia Tanzania, alisaini mkataba wake wa muda merefu, Januari 2014 na kuanza kutolewa kwa mkopo kwenye klabu mbalimbali.

Klabu ambazo amezichezea kwa mkopo Feruzi ni OFI Crete ya Ugiriki ambayo ilikuwa ikinolewa na Gennaro Gattuso, Blackpool iliyokuwa daraja la kwanza England ‘Championship’, Hibernian ya Scotland, Excel Mouscron ya Ubelgiji na Swindon Town.

Baada ya muda wake wa kumalizika wa kucheza kwa mkopo Swindon Town, Feruz amerejea tena Chelsea ambapo anaendelea kutumika kwenye timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 23.

Mafanikio makubwa ambayo ameyapata Feruz ni kushinda mataji mawili, moja likiwa la FA msimu wa 2011/12 na Kombe la Ligi Kuu England ‘EPL’ msimu wa 2013/14 akiwa na timu ya vijana ya Chelsea kwenye ngazi tofauti.