Nyota Yanga wapo kamili gado

YANGA inaendelea kujifua mkoani Morogoro ambako wameweka kambi kujiandaa na ligi pamoja na kucheza na  USM Alger, Agosti 19 Uwanja wa Taifa katika muendelezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Winga wa timu hiyo, Deus Keseke amezungumzia mandalizi kuelekea mchezo huo kwamba watafanya maajabu licha ya kwamba hawana nafasi ya kusonga mbele, huku akisisitiza kwamba wanahitaji kuweka heshima mbele ya mashabiki wao.

 

"Mandalizi ni popote sio lazima utoke nje ya nchi, kikubwa ni mwili kuuweka tayari kwa ajili ya kazi, tupo sawa kuwakabili USM Alger na tunaamini tutashinda na mashabiki wataondoka wamefurahi.

"Hiyo mechi ni muhimu kwetu kwani itawafanya mashabiki wakiamini kikosi chao kitakachofanya kazi katika msimu mpya wa 2018/19 na kikubwa tunawaza ubingwa na si vinginevyo"anasema.

Kwa upande wa Feisal Salum 'Fei Toto' amesema wanautarajia mchezo huo kutoa picha halisi ya nini wanahitaji kukifanya katika ligi inayoanza Agosti 22.

"Tunahitaji kushinda mchezo wa kimataifa, lakini pia mashabiki watahitaji kuona picha halisi ya kikosi ambacho kitawawakilisha kwenye ligi inayokuja,"anasema.