Nyota Yanga freshi

Muktasari:

  • Mwenyekiti wao, Clement Sanga akimaliza utata juu ya tuhuma za ulaji wa fedha.
  • Nyota wa Yanga tangu warejee kutoka Kenya kwenye mchezo wao wa CAF dhidi ya Gor Mahia walikuwa kwenye mgomo baridi wakisusia mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa marudiano na Wakenya hao, jambo lililowashtua mabosi hao.

MABOSI wa Yanga wajanja sana. Jana Jumapili waliamua kujifungia faragha kwa saa tatu na nyota wao, ili kuwalainisha wamalize mgomo baridi, huku Makamu

Mwenyekiti wao, Clement Sanga akimaliza utata juu ya tuhuma za ulaji wa fedha.

Nyota wa Yanga tangu warejee kutoka Kenya kwenye mchezo wao wa CAF dhidi ya Gor Mahia walikuwa kwenye mgomo baridi wakisusia mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa marudiano na Wakenya hao, jambo lililowashtua mabosi hao.

Fasta wakaamua kuitisha kikao hicho na nyota hao kilichofanya makao makuu ya klabu hiyo iliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 9:25 alasiri na baada ya hapo wachezaji walitoka wakitabasamu kwa furaha.

Viongozi walioshiriki kikao hicho ni wanene wa Kamati ya Mashindano na Usajili, chini ya Mwenyekiti wao Hassan Nyika, Mustapha Ulungu, Hussen Ndama, Mussa Katabalo, Mzee Mashauri na Meneja Hafidh Saleh.

Nyota walioshiriki kikao hicho ambacho kiliwatuliza kwa kuahidiwa neema mara baada ya mechi za CAF ni Youthe Rostand, Ramadhani Kabwili, Hassan Kessy, Said Juma ‘Makapu, Raphael Daud, Pius Buswita, Yusuph Mhilu, Said Mussa, Yohana Mkomola, Mrisho Ngassa, Deus Kaseke, Amiss Tambwe.

Wengine ni Thabani Kamusoko, Kabamba Tshishimbi, Baruan Akilimali, Godfrey Mwashuiya, Pato Ngonyani, Juma Abdul na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Mwanaspoti iliyokweka kambi Jangwani ilidokezwa kuwa ndani ya kikao mabosi waliwatuliza nyota hao kusitisha mgomo na kuahidiwa stahiki zao mapema.

Inaelezwa awali kikao kilipangwa kufanyika Jumamosi kikiitishwa na Sanga, lakini wajumbe wengi hawakuwa katika nafasi ndipo kikafanyika jana na kuweka mambo sawa, huku wachezaji hao wakiahidi kutuliza akili kuwapa raha wanayanga.

“Tumekubaliana kuwalipa wachezaji kila wanachodai kabla ya Ligi Kuu kuanza kwani hilo ndilo lilikuwa kubwa na likatufanya tukae kikao kirefu na kizito lakini tumewahakikishia kuwapa kila wanachodai ndani ya muda,” alisema mmoja ya viongozi walioshiriki kikao hicho.

“Tutawapa mishahara, posho zao zote na pesa zilizobaki katika usajili na kila stahiki ya mchezaji atapata kwa wakati kwani mambo yote yanakwenda vizuri kama tulivyokubaliana.

“Wachezaji walidai hata kufungwa na Gor kulitokana na kutokuwa vyema kisaikolojia kutokana na ishu ya stahiki zao, lakini kwa sasa wapo tayari kufanya kazi baada ya mabosi wao kuwahakikishia kila kitu ili heshima ya Yanga irudi.”

Baada ya kikao kumalizika wachezaji wote na viongozi waliondoka na wakionekana wanacheka na walielekea Kinondoni Brake Point kupata chakula cha mchana.

“Waliomaliza mikataba watapewa mipya na mambo yote yaliyokuwa yakiwatatiza yameisha,” alisema kiongozi huyo, huku mmoja ya wachezaji akikiri kwa sasa Yanga mambo ni bampa tu bampa, kwani kila kitu kipo poa.

Wakati hayo yakiendelea Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga aliamua kuanika ukweli wa taarifa zinazosambaa mitandaoni juu ya ubadhilifu wa fedha akidai huo ni upotoshaji mkubwa.

Tangu juzi kulikuwa na taarifa za kuwepo kwa ubadhirifu wa Sh440 Milioni uliofanywa na mabosi wa Yanga na eti, suala hilo limeshafika mikononi mwa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) ambao jana waliruka kimanga.

Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba aliliambia Mwanaspoti, hana taarifa hiyo, ila alikiri kuwepo na kesi nyingi za klabu za Simba na Yanga ofisini kwao.

“Hizi Simba na Yanga bwana zina kesi kesi nyingi tu huku kwetu, lakini hiyo ya ubadhirifu wa Milioni 440 sina taarifa zake,” alisema Misalaba.

Sanga alifafanua akisema taarifa hizo ni upotoshaji na zinatengenezwa ili kuigawa klabu kwa manufaa ya watu wachache.

“Yanga hivi sasa ipo katika kipindi kigumu kweli kweli kiuchumi, mtu anaweza kuchukua fedha hizo kweli? Walishindwa kuiba enzi zile Yanga ipo peponi miaka mitano iliyopita ikienda kambini Uturuki iwe sasa timu ipo hoi kiuchumi?” alihoji Sanga na kuendelea,

“Timu imeenda Kenya kucheza na Gor Mahia, watu wakitumia fedha zao mifukoni kwa mapenzi, leo hii mtu tu anaandika mtandaoni vitu visivyo na ukweli.

“Sawa tunapata udhamini wa Azam, Sh 300 Milioni kwa mwaka ila kwa matumizi ya Yanga ni fedha ya miezi miwili tu imekwisha, miezi mingine 10 tunajiendeshaje?.

“Tunakatwa asilimia 55 kwenye mapato yetu kwa ajili ya kodi ya ardhi, timu ilifikia mahali tunapata mgao wa Sh 100,000 kwenye mechi na Mwadui, ila bado tumeweza kuifikisha hatua ya makundi kimataifa, bado kuna watu hawalioni hilo.

“Wapo wanaotukana mitandaoni, wanashinikiza nijiuzulu, sawa nipo tayari kujiuzulu ila namkabidhi timu nani? Naweza kumuandikia barua Mwenyekiti wa

Bodi ya Wadhamini (George Mkuchika) kama walivyofanya wengine, ila nitakuwa nafanya kinyume na Katiba ya Yanga, sikukabidhiwa timu kwa staili hiyo. Je, Mkuchika ataiendeshaje? Hatutajenga zaidi ya kubomoa.”

Alisema fedha wanazopata kwenye udhamini kwa macho inaonekana nyingi lakini haitoshi katika kuendesha klabu tofauti na vile ambavyo watu wanafikiri na inafikia kipindi kuna watu wachache wanatumia fedha zao mfukoni.

“Yusuf (Manji) aliamua kubadili mfumo, akataka aikodishe Yanga wakasema hatumtaki aondoke, tulimtegemea sana katika kutoa fedha, sasa timu haina fedha

hakuna anayejitokeza kusaidia, ndio wanakuwa wa kwanza kupotosha mtandaoni.

ISHU YA MANJI

Kuhusu kurejea kwa Mwenyekiti wao wa zamani, mfanyabiashara Yusufu Manji, Sanga alisema kwa kinachoendelea hivi sasa inakuwa ngumu kwa mtu kujiridhisha na kuwekeza Yanga na sio Manji tu hata wadau wengine.

Pia alisema kwa jinsi hali ilivyo hata wakiitisha mkutano wa dharura ili kuweka mambo sawa bado hakutakuwa na muafaka kwani tayari kuna waliotengeneza ‘sumu’ kwa faida wanayoijua wao.

“Nimekuwa kimya muda wote, si kama nafurahishwa na kinachoendelea kwenye timu yetu la hasha, nilimfuata Mkuchika tukazungumza lakini kwa ‘situation’ iliyopo hata tukiitisha mkutano mkuu wa dharura bado kuna watakaozomea, sababu wamejipanga kuivuruga Yanga na hakutakuwa na muafaka zaidi ya vurugu.

“Nimeitumikia Yanga tangu timu ina fedha timu iko peponi hadi sasa haina fedha sijaikimbia na kwa ukata huo huo uliokuwepo timu imefika hatua ya makundi kimataifa.

Hata hivyo bado watu wanaandika upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii, hawahoji Yanga imewezaje kufika huko katika mazingira haya?