Nyota Yanga ang’ara mechi ya ndondo

Wednesday June 13 2018

 

By Stephano Simbeye

Mbozi. Mshambuliaji wa Yanga, Geophrey Mwashiuya amemekuwa kivutio kwenye michuano ya ligi ya Kimondo Day inayoendelea mjini Vwawa-Mbozi mkoani Songwe baada ya kujiunga na Klabu ya Hazundila Fc inayotokea Kijiji cha Nansama, Kata ya Isansa wilayani Mbozi.

Wachezaji wengine ni pamoja na Goephrey Mlawa ambaye msimu uliopita wa Ligi Ligi Kuu ya Vodacom alionekana Klabu  majimaji ya Songea.

Mchezaji huyo aliichezea timu ya Hanzundila FC na kufanya timu hiyo kufuzu baada ya kuitoa timu ya Tunduma City kwa mikwaju ya penati 9 – 8 baada ya timu hizo kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida za mchezo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa CCM-Vwawa.

Wachezaji wengine ni wale waliokuwa katika timu ya Kimondo SS  akiwemo Haji Pius  na Asifiwe Mashidy na wengine wanachezea timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo.

Akizungumza mara baada ya mchezo kuisha Mwashiuya alisema ameyafurahia mashindano hayo kutokana na vijana wengi chipukizi kuhamasika na hivyo kuwa chachu nyingine ya kuibua vipaji vya wanamichezo.

Alisema kwa jinsi alivyoyaona mashindano hayo yataibua vijana wengi, na kuleta hamasa kubwa ya kutangaza kimondo na Mkoa wa Songwe.

Ligi hiyo ilianza Juni 8, mwaka huu na inashirikisha timu 16 ambazo zinashindania ubingwa na kitita cha Sh2 milioni.