Nyota 10 wa kigeni Ligi Kuu, wabongo wajipange

Muktasari:

Uamuzi wa kuongeza wachezaji hao wa kigeni umekuja wakati huu wa usajili hivyo kutoa mwanya kwa klabu nyingi kuja wageni katika vikosi vyao.

Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia amesema wataongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka saba wa sasa hadi kumi na wote wanaweza kuanza katika mechi moja.

Uamuzi wa kuongeza wachezaji hao wa kigeni umekuja wakati huu wa usajili hivyo kutoa mwanya kwa klabu nyingi kuja wageni katika vikosi vyao.

"Tutaboresha kwa wachezaji wa kigeni kuwa kumi na wanaweza kutumika hata katika mechi moja hilo si jukumu letu kazi itakuwa kwa makocha, lakini TFF tumeruhusu.

"Tutaweka kanuni ngumu kwa timu kutaka kumsajili mchezaji yoyote wa kigeni ili kupata waliokuwa bora na wanastahili kuwa katika Ligi yetu tupo katika hatua za mwisho kuzipitia sheria hizo na tutaziweka wazi siku si nyingi,” alisema Karia.

"Wachezaji wapo sasa katika klabu za Ligi Kuu na hawana vigezo hivyo hatutawatoa ila walimaliza mikataba yao tunataka wasajiliwe waliokuwa na vigezo stahili na tutasimama na ukali katika hili," alieleza Karia na kuongezea hayo yalikuwa makubaliano na klabu za Ligi Kuu Bara.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau alisema walichokubaliana mpaka kuongeza wachezaji ni kuwepo ushindani katika Ligi Kuu.

Kidau alisema kuvutia wadhamini wengi kujitokeza kuzamini Ligi na hata timu zilizokuwepo na wachezaji wa wazawa kupata ushindani wa kutosha kutoka kwa wachezaji waliokamalika.

Alisema kupata wachezaji wengi wa kigeni waliokamilika wataongeza nguvu katika timu haswa kushindana na kufika mbali kwenye mashindano ya kimataifa.

"Wachezaji wa wazawa pia nao kuanza kufikilia zaidi kucheza soka la nje, na timu ya Taifa ikiitwa kuwe na wachezaji wengi kutoka nje ya Tanzania.

"Msimu uliopita ulikuwa na wachezaji wa kigeni 40 katika timu 16 sawa na asilimia nane ndio maana tumekubaliana na klabu kuongezea idadi,"alisema Kidau.