Nyie ubingwa mbona bado

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti jana, Cannavaro alisema anashangazwa na hali ya kujiamini kupita kiasi iliyojengeka kwa mashabiki na viongozi wa Simba, kuwa ni lazima msimu huu wawe mabingwa.

ACHANA matokeo ya Simba dhidi ya Lipuli ya Iringa pale Uwanja wa Samora, ambapo mastaa wake wametoka huku vichwa chini baada ya kuambulia pointi moja na kupunguzwa kasi ya kuukaribia ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Lakini, huko Yanga ambao kikosi chao kimetua jijini Mbeya kusaka pointi tatu ili kuweza kuifukuzia Simba kileleni, wamepatwa mzuka baada ya kusikia taarifa za matokeo ya wapinzani wao hao, lakini pia wakashusha angalizo. Nahodha wa Yanga na beki kisiki wa kati, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ameangalia kiu ya viongozi na mashabiki wa Simba kisha akawaambia: “Jiandaeni kisaikolojia kuna saprize za kutosha zinakuja.”

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Cannavaro alisema anashangazwa na hali ya kujiamini kupita kiasi iliyojengeka kwa mashabiki na viongozi wa Simba, kuwa ni lazima msimu huu wawe mabingwa.

Alisema Simba wanaona ligi imemalizika, lakini miongoni mwa ligi duniani ambazo hazieleweki ni pamoja na Ligi Kuu Bara hivyo, wajipange wasije kusababisha maafa pale Mitaa ya Msimbazi. Hata hivyo, aliwataka mashabiki na viongozi wa Simba kusubiri hadi mwishoni mwa msimu kuona kama watabeba taji hilo ama watachemsha badala ya kujiamini kupita kiasi.

“Sijajua kwanini mashabiki na viongozi wa Simba wanajipa ubingwa mapema kiasi hiki, unajua soka letu lina maajabu tena sana kwani, hapa kwetu mambo yako fresh lakini, tunakwenda kimya kimya ili tusiharibu mambo,” alisema Cannavaro. “Simba wamepania kila mmoja anaamini wanakwenda kuchukua ubingwa, sasa ikitokea wameukosa watasababisha maafa pale Msimbazi, wawe na subira wajifunze kusubiri na njia pekee ni kujiandaa kisaikolojia tu.”

MBEYA NI MZUKA

Yanga ilikutua mjini hapa, tayari kuikabili Mbeya City uwanjani Sokoine leo ikiwa na mzuka wa ushindi.

Kocha wao, Shadrack Nsajigwa alikasema watawapa zawadi kesho (leo) pale Sokoine. Nsajigwa alisema kwa sasa wamekuwa na ratiba ngumu, lakini kwa kuwa wanafahamu namna ya kujipanga wanaendeleza mapambano.