Nyie mpeni Sanga muone mambo

 WIKIENDI hii kutakuwa na matukio mawili makubwa. Tukio la kwanza ni la kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere keshokutwa Jumamosi.

Tukio kubwa jingine litakuwepo Jumapili ambapo Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) itapata viongozi wapya watakaoiongoza kwa kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Mchuano mkali upo katika nafasi ya Mwenyekiti ambapo Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga kwa mara ya kwanza amejitosa kuwania nafasi hiyo akichuana na Hamad Yahya ambaye anawania muhula wa pili.

Mwanaspoti limefanya mahojiano ya kina na Sanga kuhusu dhamira yake ya kugombea nafasi hiyo nyeti kwenye soka la Tanzania.

Kama ulikuwa hufahamu ni kwamba Bodi ya Ligi ndiyo inayosimamia Ligi Kuu pamoja na Ligi daraja la kwanza (FDL) na la pili (SDL).

“Nimeona Bodi ya Ligi kuna upungufu mkubwa hasa katika usimamizi wa soka letu. Kuna mambo hayaendi sawa hivyo inahitajika mtu makini anayeweza kusimamia, naamini ninaiweza kazi hiyo vizuri,” anasema Sanga ambaye amekuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga tangu 2012 hadi Mei mwaka huu alipokaimu nafasi ya Mwenyekiti.

“Mfano Bodi ya Ligi haijatembelea klabu za Ligi Kuu kwa muda mrefu ili kuweza kufahamu ni changamoto gani wanakutana nazo. Nikipata nafasi nitaweka kalenda kabisa ya kuwatembelea. Unajua hawa ndiyo wenye ligi, ni lazima kuwasikiliza na siyo kusubiri mpaka kipindi cha uchaguzi ndiyo uende,” anaeleza.

UFUMBUZI WA MATATIZO

Moja ya vitu ambavyo Sanga anaamini, vinamfanya kuwa mtu sahihi katika nafasi hiyo ni namna ambavyo baadhi ya matatizo yamekosa ufumbuzi na yanatakiwa kutatuliwa mapema.

“Hali ya baadhi ya timu kiuchumi ni mbaya, bodi inatakiwa kusaidia katika kutafuta wadhamini wengi zaidi katika Ligi. Mfano mkataba wa Vodacom unaelekea ukingoni sasa lakini hakuna juhudi zilizofanyika kuhakikisha tunapata udhamini mapema.

“Nimezungumza na watu kama SportPesa na wameonyesha nia ya kusaidia mpira wetu, wanasema wana nia ya kuidhamini Ligi Kuu, lakini anahitaji kiongozi makini wa kusimamia,” anasema Sanga ambaye anasifika kwa kuwa na misimamo.

“Tatizo kubwa katika upande wa wadhamini ni kwamba hatujawa na kitengo maalumu cha kutafuta wadhamini. Watu ambao wataitengeneza Ligi kama bidhaa na kuweka thamani yake juu. Kwa sasa wadhamini wanakuja na bei zao, tunakuwa wa bei rahisi,” anasisitiza.

“Tumekuwa na matatizo mengine katika usimamizi wa Ligi. Mfano leo matamasha ya muziki yanapangua ratiba ya Ligi Kuu. Tunatakiwa kuwa na ratiba moja, kwanini hawa wa matamasha wasiombe viwanja mapema ili kuondoa mgongano na kuwa na ratiba iliyotulia.

“Katika utunzaji wa kumbukumbu pia utaratibu haukuwa mzuri. Kwa sasa nimeona tumekuwa na tovuti lakini bado imekuja kwa kuchelewa. Tulihitaji kujipanga mapema zaidi,” anasema swahiba huyo wa Yusuf Manji.

CHANGAMOTO NYINGINE

Sanga anazitaja changamoto nyingine zinazoikabili Ligi Kuu kuwa ni pamoja na viwango vya chini vya baadhi ya waamuzi na ubora wa viwanja lakini atahakikisha ufumbuzi unapatikana.

“Kwa waamuzi ni wazi kwamba kuna matatizo lakini bado kuna maswali ya kujiuliza. Hawa Waamuzi wanapata mafunzo mara ngapi kwa mwaka? Wanapata semina elekezi mara ngani kwa mwaka ili kuwasaidia viwango vyao.

“Tunatakiwa kutengeneza njia ya kuwasaidia hawa waamuzi ili wawe na viwango vizuri zaidi ya sasa,” anaeleza Sanga ambaye katika kipindi cha miaka mitano ambayo amekuwa kiongozi wa juu wa Yanga, klabu hiyo imeshinda mataji manne ya Ligi Kuu.

Akizungumzia vitendo vya baadhi ya kamati kushindwa kuwa na maamuzi sahihi ama kuchelewa kutoa uamuzi, Sanga anasema akipata nafasi ya uongozi atahakikisha anaziwezesha kamati hizo kuwa na ufanisi na uwezo mkubwa wa kusimamia sheria.

“Unajua mashauri ya kinidhamu na mengine yanasimamiwa na Kamati ambazo ziko huru. Bodi inatakiwa kuziwezesha kamati hizi kufanya kazi kwa wakati na kusimamia sheria inavyopaswa,” anasema.

RATIBA IMARA

“Inashangaza kuona tunakuwa na ratiba inayobadilika kila mara. Wakati mwingine unaweza kuona ratiba inaonyesha timu fulani iko nyumbani katika mechi tano ama zaidi, huu sio weledi,” anaanza kueleza.

“Mfano msimu huu pamoja na kelele nyingi tunahitaji kuwa na ratiba inayoeleweka bado ilibadilika baada ya mechi moja tu. Ni kwetu tumeshindwa? Hii ndiyo sababu nasema tunahitaji viongozi wapya ndani ya bodi, hawa waliopo wamefikia sehemu wanashindwa kusimamia vitu.

“Kama tukitengeneza ratiba kisha tukaipeleka kwenye klabu kubaini mapungufu yaliyopo tunaweza kuwa na ratiba iliyosimama zaidi. Tutakuwa na mfumo huo, klabu ndiyo wadau wakubwa na ndiyo wanapaswa kushiriki katika kuandaa ratiba ambayo haitakuwa na matatizo,” anaeleza.

“Tunahitaji pia kuwa na mafunzo kwa viongozi wa klabu na wadau wengine pia kama Waandishi wa Habari ili kuhakikisha wanasimama katika weledi wao,” anaongeza.

ELEKTRONIKI, TFF

Sanga anafichua kuwa kunahitajika mabadiliko kadhaa katika mfumo wa mapato tulionao ili kuwepo kwa uwazi wa kiwango cha fedha kinachopatikana na matumizi yake.

“Kuna mtu anafahamu mfumo wa elektroniki unakusanya kiasi gani cha fedha? Nani anahoji mapato? Hayo ni mambo ambayo inabidi yarekebishwe.

“Kuna mwingiliano kidogo kati ya TFF na Bodi hasa katika uwepo wa Kamati ya Mashindano ambayo ina majukumu yanayofanana na yale ya bodi ya Ligi. Bodi inatakiwa kuwa huru,” anasema.