Nyie chongeni: Katwila aisubiri Simba Mwanza

Muktasari:

  • Kuelekea mchezo huo, mashabiki na wanachama wa Simba  katika jijini la Mwanza wameshaanza vikao vya hapa na pale  kujiandaa na mapokezi ya timu yao kuhakikisha inashinda mchezo huo.

Mwanza. Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema kelele za mashabiki wa Simba hazimtii presha dakika 90 zitaamua mechi yao ya Ngao ya Jamii Agosti 18 kwenye Uwanja wa Kirumba Jijini Mwanza.

Kuelekea mchezo huo, mashabiki na wanachama wa Simba  katika jijini la Mwanza wameshaanza vikao vya hapa na pale  kujiandaa na mapokezi ya timu yao kuhakikisha inashinda mchezo huo.

Akizungumzia mchezo huo kocha Katwila amekaa na kusikiliza tambo hizo za mashabiki wa Simba alisema hatishiwi na kelele za wapinzani hao isipokuwa watulie wakutane uwanjani awaonyeshe kazi.

Alisema anaendelea kuwaandaa vyema vijana wake katika kambi yao Turiani mkoani Morogoro na kwamba ishu za Uturuki na majina ya wachezaji hayampi tabu.

“Niwaambie tu waache kelele, wasubiri tukutane uwanjani niwaonyeshe kazi, sisi Mtibwa bado tupo Manungu Morogoro, ishu za kambi ya Uturuki sijui Okwi, Kagere kitu gani? alihoji kocha huyo.

Katwila aliongeza wanatarajia kuwasili Jijini Mwanza siku tatu kabla ya pambano wakiwa na kikosi chake kamili na kwamba matarajio yake ni kushinda mchezo huo.

“Tunatarajia kutua Mwanza aidha wiki moja kabla au siku tatu kuelekea mchezo huo nikiwa na kikosi changu chote cha kazi na matarajio yangu ni kushinda mapema tu,” alitamba Katwila.