Nyie Bocco na Mkude mmemsikia Mgosi?

Muktasari:

  • Mgosi alitangazwa na Kocha wa Dodoma, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kusajiliwa dakika za mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili, huku akitamba kuwa uzoefu wake na wale waliopo kikosini utaisaidia kuipandisha timu VPL.

MUSSA Hassan Mgosi aliyekuwa akikinoa kikosi cha Simba B, ameitosa timu hiyo na kutua Dodoma FC kuichezea katika Ligi Daraja la Kwanza, huku akiwashtua kimtindo nyota wa Simba ili wajipange vema.

Mgosi alitangazwa na Kocha wa Dodoma, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kusajiliwa dakika za mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili, huku akitamba kuwa uzoefu wake na wale waliopo kikosini utaisaidia kuipandisha timu VPL.

“Tumemsajili Mgosi na ataonekana kwenye jezi ya Dodoma wakati Ligi daraja la Kwanza itakapoendelea tena,” alisema Julio.

Lakini, Mgosi akitua Dodoma iliyopo nafasi ya pili katika Kundi C, straika huyo wa zamani wa JKT Ruvu, Simba, Mtibwa na Taifa Stars alizungumza na Mwanaspoti kabla ya kuwashtua nyota wa Simba kwa kuwataka wajipange.

Mgosi aliyeichezea kwa mafanikio timu hiyo kabla ya kuwa meneja na mwaka huu kuhamishiwa timu ya B ili kuwapika vijana, amewakumbusha nyota wa timu hiyo wakiongozwa na Jonas Mkude, John Bocco na wengine kuwa, lazima wabadilike na kupambana ili msimu wa 2017-2018 umalizike salama.

Alisema wasiridhike na nafasi iliyopo timu yao kwa sasa katika Ligi kwa sababu ligi bado mbichi na badala yake waongeze juhudi huku pia wapige hesabu mechi za FA, Mapinduzi Cup na Kombe la Shirikisho Afrika.

“Kila wakati lazima utathimini malengo yako kama yametimia, hivyo nyota wa Simba wajipange kuumaliza mwaka 2017 salama na kuingia mwaka 2018, lazima waanzie hapo,” alisema Mgosi.