Nsajigwa hataki zaidi ya ubingwa VPL

UNGUJA. PENALTI mbovu ya straika matata wa Yanga, Obrey Chirwa iliiondosha klabu hiyo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi juzi Jumatano lakini kocha msaidizi wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa ameshusha pumzi.

Nsajigwa ambaye ndiye alikuwa anakinoa kikosi hicho katika mashindano hayo kutokana na kocha mkuu, Geogre Lwandamina kuwa na matatizo ya kifamilia, alisema sasa hasira zao ni kwenye Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).

“Tumeshasahau yaliyopita na sasa tunaangalia mbele, hasa katika Ligi Kuu ambapo tumeachwa pointi tano na vinara Simba. Tunatazama jinsi gani tunaweza kupata matokeo ya ushindi na kuwapita kama ilivyokuwa msimu uliopita,” alisema.

“Nguvu yetu kama timu sasa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na pia tufanye vizuri katika mashindano ambayo tupo kama kombe la FA, ambalo msimu uliopita tuliishia hatua ya nusu fainali, pia mashindano ya kimataifa,” alisema.

Wakati huo huo kocha mkuu, Lwandamina ambaye alikuwa jukwaani wakati Yanga ikiondoshwa na URA kwa mikwaju ya penalti, alisema ameona upungufu katika timu na kuahidi kuufanyia kazi fasta.