Njombe Mji yaichapa Mbao

Monday November 13 2017

 

By Justa Musa

Mbeya.Njombe Mji imeichapa Mbao FC kwa bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Aman Makambako.

Katika mchezo huo bao la ushindi la Njombe Mji lilifungwa na chipukizi Cassimu Yusuph  ‘Ronaldo’ katika dakika 74.

Njombe Mji ipo katika maandalizi ya mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe Jumamosi ijayo.

Mbao FC ipo mkoani Njombe kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya mechi yao watakayokuwa ugenini dhidi ya Majimaji FC ‘Wanalizombe’ kwenye Uwanja wa Majimaji Novemba 18 mwaka huu

Kocha wa Njombe Mji, Mrage Kabange alisema mechi hizo ni kipimo kwa kikosi chake kabla ya kuivaa Azam.

Alisema wakati wa kipindi hiki ligi ilivyosimama kwa muda kupisha ratiba za Soka kimataifa (FIFA) tumetumia kwa kucheza mechi za kirafiki.

“Tumepata sare kadhaa tukiwa katika uwanja wa nyumbani kitu ambacho hakipingiki kwani soka lina matokeo matatu ya kufunga, sare na kufungwa, lakini kwa wadau na wapenzi wa timu hii wameonyesha kutofurahia hali hiyo,’’alisema Kabange   

Kabange alisema baada ya kucheza na Mbao FC, leo wanatarajia kuwa na mechi nyingine ya kirafiki wilayani Mbarali kucheza na Ihefu FC inayoshiriki ligi daraja la pili kitaifa (SDL).