Niyonzima atawashangaza wengi

Muktasari:

 Niyonzima tangu alipotua Simba amekuwa akiandamwa na majeruhi ya mara kwa mara

Dar es Salaam. Kocha wa Mwadui FC, Ali Bizimungu amemtaja kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima kuwa ni mmoja ya wachezaji moto atakaporejea tena uwanjani.

Bizimungu alisema alianza kumfuatilia Niyonzima akicheza Uganda na kumuona ni mchezaji mwenye mbinu na asiye muoga uwanjani, sambamba na uwezo wake mzuri wa kutoa pasi za mwisho na kudai hata sasa moto huo bado anao.

"Bado Niyonzima ni mzuri, ninacholishauri benchi la ufundi la Simba, akirejea wamjenga kiakili, ili asipoteze utulivu na hilo ndilo linalowashinda wengi na kujikuta wakipoteza wachezaji wazuri ambao wangeisaidia timu kufika mbali," alisema kocha huyo.

Kuhusu timu yake ya Mwadui alisema imefika ilipo kwa sasa chini yake kwa sababu ya nidhamu na kujituma kwa vijana wake uwanjani na kudai anajipanga kwa mechi zao zijazo za nyumbani ili kuhakikisha wakaa pazuri.

Mwadui itacheza mechi tano mfululizo wakiwa nyumbani dhidi ya Majimaji, Stand United, Mbao, Lipuli na Yanga.