Niyonzima, Okwi waitesa Simba

Friday January 12 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN

Dar es Salaam. Hali bado si shwari sana ndani ya kikosi cha Simba baada ya wachezaji wake Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima kushindwa kufanya mazoezi na timu hiyo inayojiandaa na mechi dhidi ya Singida United.

Simba inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Bandari Temeke chini ya kocha Masoud Djuma mwenye lengo la kushinda mechi yake dhidi ya Singida United ili kurudisha amani na imani ndani ya klabu hiyo baada ya kufanya vibaya katika Kombe la Mapinduzi.

Niyonzima na Okwi walikosekana katika kikosi cha Simba kilichoshiriki  mashindano ya Mapinduzi na kuambulia kutolewa katika hatua ya makundi.

Okwi amekuwa nje ya kikosi hicho kwa muda mrefu kutokana na kuwepo kwa madai kuwa anamahitaji yake binafsi bado hajatimiziwa na uongozi wa Simba.

Suala la Okwi limeonekana kuwa juu ya kocha Djuma kwani hata viongozi wa Simba wameshindwa kuweka wazi kwani mchezaji huyo ameshindwa kuungana na kikosi hicho kwa zaidi ya mwezi sasa.

Mwenyekiti wa kamati ya usajili Simba, Hans Poppe alisema taarifa alizonazo Okwi bado anaendelea na matibu na si vinginevyo kama baadhi ya watu wanavyosema anadai fedha zake za usajili.

“Nilivyopata habari Okwi ni kwamba alikuwa anauguza shingo huko kwao sasa kama hayupo ni kwa sababu ya kuumwa”-Hans Poppe.

Naye Niyonzima alisema bado hajapona na anaendelea mazoezi kidogo kidogo huku akiwa chini ya uangalizi wa daktari wake ndio atampa ruksa ya kurudi uwanjani.

"Nafanya mazoezi mwenyewe sijasikia uwezo wa kufanya na timu kwani bado sijawa fiti kiasi kikubwa ndio maana nafanya mazoezi yangu madogo chini ya uangalizi, " alisema kiungo huyo.

" Kuhusu kuwepo kwenye mechi dhidi ya Singida United,  sijajua kwani maendeleao yangu yanaendelea kuwa vizuri, lakini taratibu taratibu na kama daktari ataniruhusu sawa nitarudi uwanjani, lakini kama nitakuwa bado basi nitaendelea na mazoezi, " alisema Niyonzima.