Niyonzima, Juuko wajifua Simba

Muktasari:

  • Nyota hao wa Rwanda na Uganda walikuwa nje ya kikosi hicho tangu kuanza kwa msimu huu

Dar es Salaam. Nyota wa Simba, Haruna Niyonzima na Juuko Murshid wamejifua kwa mara ya kwanza katika kikosi cha mabingwa hao watetezi katika mazoezi yaliyofanya kwenye Uwanja wa Boko Veterans.

Niyonzima na Juuko wamejiunga na kikosi hicho baada ya kumaliza tofauti zao viongozi wa klabu hiyo.

Simba inajiandaa na mechi zake mbili za kanda ya ziwa dhidi ya Mbao na Mwadui ilifanya mazoezi chini ya makocha Patrick Aussems, Masoud Djuma na Adel Zrane.

Kabla ya mazoezi kuanza Niyonzima na Juuko waliongea na Aussems mazungumzo yasiozidi dakika mbili na baada ya hapo kila mmoja alimaliza kwa kucheka na kujiunga na wenzao kuanza mazoezi ambayo yalianza saa 10:00 jioni.

Kocha Zrane alitumia muda mwingi na wachezaji Juuko na Niyonzima walioanza kwa kufanya mazoezi wenyewe kabla ya kujiunga na timu.

Niyonzima na Juuko waliwekwa katika kundi la wachezaji ambao hawakusafiri na timu kwenda Mtwara na wale ambao waliingia kipindi cha pili na wale ambao hawakucheza kabisa katika mechi hiyo.

Kundi hili lilikuwa likisimamiwa na makocha Aussems na msaidizi wake Masoud Djuma na mazoezi waliyokuwa wakifanya ni kupasiana pasi kwa haraka zaidi huku wakiwa katika makundi mawili tofauti.

Niyonzima alionyesha kuwa bado yupo katika kiwango na ubora wake kwa kupiga pasi nzuri na haraka kama Aussems alivyokuwa anataka na muda mwingine alipiga zile za kisigino kama ilivyo kawaida yake. 

Niyonzima hakuishia hapa aliwapoteza wachezaji wa kundi lingine ambalo walikuwa wakimkaba na muda mwingine alikuwa akipiga pasi zake za madaha mwili na uso unageuka upande mwingine na mpira unakwenda kwingine asipokuwa anaangalia.

Juuko alikuwa katika kundi moja na Niyonzima na alionyesha ubora wake wa kukaba pindi wanapopoteza mpira na alikuwa anapora mipira mara nyingi pindi anapousaka.

Juuko alikuwa akifanya na hivyo na alifanikiwa kupora mipira mara kwa mara na kumfanya kocha Djuma muda mwingine kutoa kauli kwa kumwambia "safi, fanya zaidi ongeza Juuko," alisikika Djuma.

Kundi la Niyonzima lilikuwa na Juuko, Said Ndemla, Adam Salamba, Nicholas Gyan, Rashid Juma na Poul Bukaba.

Wengine walikuwa Yusuph Mlipili, James Kotei, Cletus Chama, Mohammed Rashid, Abdul Selemani na Marcel Kaheza.