VIDEO: Niyonzima, Juuko waingia mitini

Thursday August 9 2018

 

By THOMAS NG’ITU

NYOTA wa kimataifa wa Simba, Juuko Murshid na Haruna Niyonzima, wameingia mitini katika Tamasha la Simba Day baada ya kukosekana Uwanja wa Taifa.

Wakati wa utambulisho nyota wa kikosi kipya cha Simba, wengi walitarajia kuwaona ama kusikia majina yao lakini hali ilikuwa tofauti.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alimaliza kuita orodha ya wachezaji hao kwa kuhitimisha kwa jina la mshambuliaji John Bocco, hali iliyofanya mashabiki kuanza kujiuliza kuhusu wachezaji wao Niyonzima na Juuko na hata kipa Said Mohammed ‘Nduda’ na Emmanuel Mseja ambao walielezwa na vioongozi hawajaachwa.

Awali iliripotiwa Niyonzima yupo nyumbani kwao Rwanda licha ya kukatiwa Visa ya kwenda nchini Uturuki huku Juuko Murshid ambaye alikuwa akifanya majaribio Afrika Kusini na akikosekana uwanjani hapa.

Hali hiyo imezidi kuzua hoja kwa mashabiki kwani wamejikuta wakiulizana maswali yasiyo na majibu kama wachezaji hao bado ni wa kwao au vipi.

Kabla ya Simba kutambulishwa vikosi vya Simba Queens na kile cha U20 waliopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Dodoma ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kilitambulishwa sambamba na benchi zima la ufundi la Msimbazi.