Ninje kapanda mzuka kinoma

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Meneja Uhusiano wa Hifadhi hiyo, Joyce Mgaya, alisema udhamini wao umetokana na uzalendo walionao huku wakiitaka timu hiyo kusonga mbele zaidi katika mashindano yao.

KOCHA Amy Ninje anayekinoa kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20, ‘Ngorongoro Heroes’, amejikuta akiogelea manoti baada Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, kuidhamini safari yao ya kwenda DR Congo huku ikijipanga kuwa wadhamini wakuu wa timu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Meneja Uhusiano wa Hifadhi hiyo, Joyce Mgaya, alisema udhamini wao umetokana na uzalendo walionao huku wakiitaka timu hiyo kusonga mbele zaidi katika mashindano yao.

“Timu yetu ya vijana inashiriki mashindano makubwa kwa hiyo tutaitangaza hifadhi yetu, tumeanza kuidhamini safari yao kwenda DR Congo lakini tunataka tuidhamini kabisa timu yetu hii ya Taifa, hivyo huu ni uzalendo mkubwa kwetu tuliouonyesha na kuitaka timu isonge mbele,” alisema.

Naye Ninje amesema udhamini huo umewaongezea morali wachezaji wake kuelekea mechi yao ya marudiano dhidi ya Congo.

Kuhusu mchezo huo utakaopigwa April 22, alisema kwamba, waliweka kambi kwa muda mrefu na wamefanikiwa kupata mfumo mwingine ambao utawasaidia katika kutafuta ushindi nchini Congo.

“Mchezo huu una umuhimu kwetu kwa hiyo tumefanya marekebisho mengi hasa katika upande wa ushambuliaji, tunaamini kabisa katika mchezo huu tutatoka na ushindi,” alisema huku akiitakia kheri kwa kuwa Ngorongoro inatakiwa ushindi au sare ya mabao.