Ni Vita ya Manula, Odhoji kipa bora Sportpesa

Muktasari:

  • Stori zinasema kuwa kuna vita kubwa kati ya Kipa wa Kogalo, Shaban Odhoji na Kipa wa Wekundu wa Msimbazi, Aishi Manula, unajua ni kwanini?

Nakuru. Kuelekea mechi ya fainali ya Sportpesa Super Cup, utakaonguruma kesho kuanzia saa 9 alasiri, ugani Afraha, tayari presha imeanza kupanda kunako kambi ya Gor Mahia na Simba SC. Unaambiwa ni Vita mazee!

Stori zinasema kuwa kuna vita kubwa kati ya Kipa wa Kogalo, Shaban Odhoji na Kipa wa Wekundu wa Msimbazi, Aishi Manula, unajua ni kwanini?

Wanaume hawa mpaka sasa wamekabana koo katika rekodi ya 'clean Sheet'. Naam, hadi kufikia mechi ya fainali itakayorindima kesho Juni 10, mjini hapa, siyo Aishi Manula wala Shaban Odhoji aliyeruhusu nyavu zake kutobolewa ndani ya dakika 90.

Katika mechi ya robo fainali, Manula alisimama langoni na kuishuhudia Simba ikilazimisha suluhu dhidi ya Kariobangi Sharks, kabla ya kuwatandika kwa matuta. Baadaye katika mechi ya nusu fainali, kipa huyo tena alifanikiwa kuwazuia wababe wa Yanga, Kakamega Homeboyz. 

Simba wakatinga fainali. Hali ilikuwa vivyo hivyo kwa Odhoji. Kipa huyu mtaratibu, alisimama langoni Kogalo ilipowaadhibu JKU 3-0 kabla ya kuendeleza makali yake katika ushindi wa 2-0, dhidi ya Singida United.

VITA YA KIATU CHA DHAHABU

Vita ya kuwania kiatu cha dhahabu, inaongozwa na mshambuliaji hatari wa Gor Mahia, Mnyarwanda Meddie Kagere, akiwa na mabao matatu. Kagere alitupia mara mbili katika ushindi wa 2-0 walioupata dhidi ya Singida United, kwenye hatua ya nusu fainali ya pili, iliyopigwa Juni 7, mwaka huu. 

Straika wa Kakamega Homeboyz, Allan Wanga ana mabao mawili bado ana matumaini makubwa ya kumpiku Kagere katika mbio hizo, atakapoingia uwanjani kuwakabili Singida United, kwenye mechi ya kusaka mshindi wa tatu.

Mwaka 2017, Kagere alitupia mara tatu na kubeba kiatu cha dhahabu huku akiiongoza Gor Mahia kutwaa ubingwa wa makala ya kwanza ya Sportpesa Super Cup, walipoifunga AFC Leopards 3-0 Jijini Dar Es Salaam.

 

Wafungaji bora:

Meddie Kagere -3

Allan Wanga -2

George Odhiambo -1

Wycliffe Opondo -1

Kipa bora 'Clean Sheets':

Aishi Manula -2

Shaban Odhoji -2

Peter Manyika -1

Michael Wanyika -1

Jeff Oyemba -1