Ni Simba pekee inafagilia ishu ya mapro wa kigeni

HABARI ndio hiyo. Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limepitisha ruksa ya usajili wa mapro 10 wa kigeni badala ya saba wa awali, lakini inaonekana ni Simba pekee ndio inayofagilia mchongo huo, huku klabu nyingine zikipotezea kwa kuona wala sio ishu kubwa kwao kwa sasa.

Simba inahitaji kufanya usajili wa maana kwa vile inajiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Yanga, Singida United na Azam FC zilizokuwa vinara kwa kusajili nyota wa kigeni zikipotezea kwa vile hazina jukumu hilo msimu ujao.

Katika kikao cha pamoja cha kupitisha mchakato huo kati ya viongozi wa klabu na TFF, ambapo viongozi wa klabu 20 zitakazoshiriki ligi msimu ujao walishirikishwa, kura ziligawanyika nusu kwa nusu ambapo nusu walipitisha na nusu walipinga, ingawa baadaye Singida United ilibadili mawazo na kuyakubali mabadiliko.

Hata hivyo Mwanaspoti imezungumza na klabu juu ya uamuzi huo wa TFF na maoni yao yalikuwa hivi;

SINGIDA UNITED

Mmoja wa Wakurugenzi wa Singida United, Yusuph Mwandami, amesema wao wana mpango wa kupunguza nyota wa kigeni baada ya kubaini jamaa hao ni pasua kichwa.

“Wanaotaka suala hili ni Simba pekee nao ni kwa vile wana michuano ya kimataifa, ila kwa ushauri wangesubiri hata dirisha dogo ndipo wawasajili kwa idadi hiyo, Simba hii si ya kuwategemea akina Meddie Kagere ama Paschal Wawa kimataifa.

“Tunafikiri kupunguza tulionao hadi wanne ama watatu, wageni kwanza wana matatizo sana ambayo watu hawayajui, ndio maana hatuna mpango wa kusajili wachezaji 10.”

Kubwa alisema ni gharama wa kuwahudumia na kuwalipa, ilihali fedha hizo zinaweza kusaidia vipaji vya wazawa kwa manufaa ya taifa.

AZAM FC

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, alisema: “Upande wa faida kwa kuongeza nyota wengi wa kigeni mimi sioni kwani timu nyingi ambazo zinasajili wachezaji hao tunawaona wengi wakiwa hawana viwango, wanaletwa na viongozi ambao wanalazimisha makocha wawatumie hata kama hawapo katika mipango ya kocha.

“Kuwa na wimbi kubwa la wachezaji wa kigeni tunapoteza wale wazawa na shida kubwa tutakuja kuipata pale ambapo tutakuwa tunaita timu ya Taifa.

“Upande wetu tutatumia wageni lakini hawatawazidi idadi wazawa kwani tunaamini uwezo wao na hata katika nafasi kumi za kusajili sidhani kama tutatumia zote.”

SIMBA

Kocha wa Simba, Masoud Djuma alisema: “Tuna mashindano mengi mbele yetu, hivyo hili suala kupitishwa naona wamefanya jambo jema, tunapata nafasi ya kuwa na uwanja mpana jinsi ya kuwatumia wachezaji kulingana na mashindano.

“Kwenye kikosi chetu ni lazima tuache nafasi hata mbili au tatu kwa ajili ya baadaye kwani huwezi kujaza nafasi zote kwa wakati mmoja wakati hujui nini kitatokea baadaye, kuna kuumia na mambo mengine, hivyo tutasajili lakini sio kujaza nafasi zote 10. Ila nawapongeza sana TFF kupitisha hili na itatusaidia huko mbele.”

YANGA

Yanga ina mambo mawili makubwa ya kutosajili nyota 10 wa kigeni na hayo yanajulikana. Kwanza aina mashindano yoyote ya kimataifa mwakani, pili wanakabiliwa na ukata ambapo hata wachezaji wa ndania wameshindwa kumalizana nao sasa.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ndani ya Yanga ameliambia Mwanaspoti akisema: “Ukiangalia kwa upana hata kama hatuna pesa, lakini hatuna presha yoyote mwakani kwamba tutashiriki mashindano ya kimataifa, tunaachana na mpango huo labda tutazifanyia kazi hapo baadaye, ila kwa sasa hatuna mpango huo.”

IMEANDIKWA NA MWANAHIBA RICHARD, THOBIAS SEBASTIAN NA OLIPA ASSA