Ngorongoro Heroes yashikwa nyumbani

Dar es Salaam. Taifa ya vijana Tanzania U20 'Ngorongoro Heroes' imejiweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2019, baada ya kulazimishwa suluhu na DR Congo.

Matokeo hayo yameiweka Ngorongoro Hereoes katika mazingira magumu ya kusonga mbele wakitakiwa kushinda ugenini katika mchezo wa marudiano ili kusonga mbele.

Licha ya kiwango kizuri cha Ngorongoro Heroes, lakini ilikosa mbinu mbadala za kupenya ukuta wa DRC ambayo ilijaza idadi kubwa ya wachezaji kwenye safu ya ulinzi.

Timu hiyo ilitawala mchezo muda mrefu, lakini ilishindwa kutengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao ingawa pia ilishindwa kutumia chache ilizopata.

kupata ushindi ambao ungeiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata.

Ngorongoro Heroes ilikosa mbinu za kuingia ndani ya eneo la hatari la DR Congo kuleta madhara, hivyo ililazimika ikitumia mbinu ya kucheza mipira ya juu ambayo iliokolewa na mabeki au kuwa kona ambazo hazikuzaa matunda.

Ingawa Ngorongoro ilianza mechi kwa utulivu ilijipa muda wa kuwasoma wapinzani wao walioanza kwa kumiliki mpira, iliwachukua takribani dakika 15 kubadilika na kuwalazimisha DRC kuanza kucheza kwa kujilinda.

Hata hivyo, viungo wa Ngorongoron Heroes walishindwa kupenyeza mipira kwa washambuliaji Paul Peter na Abdul Selemanu ambao walijikuta wakishindwa kuleta madhara langoni mwa DR Congo.

DR Congo ilionekana kunufaika na stamina ndogo ya wachezaji wa Ngorongoro Heroes ambao mara kwa mara walijikuta wakizidiwa nguvu walipokuwa wakiwania mpira.

Timu hiyo ilionekana kulazimisha kupenya kupitia upande wa kulia kwa winga Said Musa aliyekuwa mwiba kwa mabeki wa DR Congo ambao walimchezea madhambi mara kwa mara ili kumpunguza kasi.

Kipindi cha kwanza nusura timu hiyo ipate penalti baada ya Musa kuangushwa mara mbili ndani ya eneo la hatari, lakini mwamuzi Wiliam Oloya kutoka Uganda alipeta.

Mshindi wa mechi hizo mbili atafuzu raundi ya kwanza ya mashindano hayo ambako ataana na Mali kusaka tiketi ya kuingia raundi ya pili  ambayo ni hatua ya mwisho kabla ya fainali hizo zilizopangwa kuchezwa mwakani nchini Niger.