Ngorongoro Heroes yaahidiwa zawadi nono

Muktasari:

Timu hiyo inasaka tiketi ya kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali ya Mataifa Afrika kwa vijana U20

Dar es Salaam.Timu ya Taifa cha Vijana Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes itaondoka kesho alfajiri kuelekea DR Congo tayari kwa mchezo wa marudiano dhidi ya wenyeji wao utakaopigwa Aprili 22.

Kocha Mkuu Ngorongoro Heroes, Ammy Ninje alisema wanatarajia kutoka na ushindi katika mchezo huo wa marudiano, baada ya kufanikiwa kurekebisha makosa waliyoyafanya katika mchezo wa kwanza.

“Mchezo huu una umuhimu kwetu kwahiyo tumefanya marekebisho mengi hasa katika upande wa ushambuliaji, tunaamini kabisa katika mchezo huu tutatoka na ushindi ili kuweza kusonga mbele zaidi,” alisema Ninje.

Wakati huo huo Hifadhi ya Ngorongoro Crater, imeidhamini safari ya timu hiyo kuelekea Congo, huku wakiweka wazi nia yao ya kuwa wadhamini wakuu katika timu hiyo.

 Kaimu Meneja Uhusiano wa Hifadhi hiyo, Joyce Mgaya alisema udhamini wao umetokana na uzalendo walionao huku wakiitaka timu hiyo kusonga mbele zaidi katika mashindano yao.

“Timu yetu ya Vijana inashiriki Mashindano makubwa kwa hiyo tutaitangaza hifadhi yetu, tumeanza kuidhamini safari yao kwenda Congo, lakini tunataka tuidhamini kabisa timu yetu hii ya Taifa, hivyo huu ni uzalendo mkubwa kwetu tuliouonyesha na kuitaka timu isonge mbele,” alisema.

Kocha Ninje alisema udhamini huo umewaongezea morali wachezaji wake kuelekea mechi yao ya marudiano dhidi ya Congo.

Ngorongoro wanatakiwa wapate ushindi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Dr Congo baada ya mchezo wa awali kutoka sare ya bila kufungana, ili kuzidi kujihakikishia nafasi ya kufuzu kuelekea katika fainali za Afcon kwa timu za Vijana zitakazofanyika mwakani nchini Niger.