Ngoma akabidhiwa jezi ya mabao Azam

Muktasari:

Ngoma ni miongoni mwa wachezaji wa Azam watakaoiwakilisha timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huu.

Dar es Salaam.  Azam FC wanachekelea sana, na hii ni baada ya kuhakikisha wamemtia kwenye himaya yao straika Mzimbabwe Donaldo Ngoma na sasa wamemtengea jezi maalumu ili aweze kuwapigia mabao vizuri.
Klabu hiyo ambayo inamilikiwa na Kampuni ya Bakhresa, imemwandalia Ngoma jezi namba 11, kama aliyokuwa anaitumia ndani ya klabu za Yanga pamoja na Platinum alikocheza kabla.
Awali, ndani ya klabu ya Azam jezi hiyo ilikuwa inavaliwa na Mghana Yahaya Mohammed, aliyerejea timu yake ya zamani ya Aduana Stars ya nchini kwao.
Azam imewasisitizia mashabikiwa wao wawe watulivu katika kipindi hiki na kuendelea kuiunga mkono timu yao kwani uongozi umejipanga kufanya kazi bora na kisasa kutokana na mapendekezo ya benchi lao la ufund.
Ngoma ni miongoni mwa wachezaji wa Azam watakaoiwakilisha timu hiyo katika michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kufanyika kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huu.
Mshambuliaji huyo amemalizana na Azam baada ya kuachana na Yanga mwanzoni mwa mwezi Mei.