Ngoma aongezewa makali huko Uganda

Muktasari:

  • Azam ipo kambini Uganda na inaendelea na mazoezi na mechi zake za kirafiki, lakini Mzimbabwe huyo mchezaji huyo amekuwa pembeni katika michezo hiyo.

STRAIKA mpya wa Azam FC, Donald Ngoma, amepewa programu maalumu huko kambini Uganda ili aweze kuwa fiti kiasi cha kurejea katika makali yake aweze kuzipenya ngome za wapinzani wao wa Ligi Kuu Bara wakiwamo Simba na Yanga.

Azam ipo kambini Uganda na inaendelea na mazoezi na mechi zake za kirafiki, lakini Mzimbabwe huyo mchezaji huyo amekuwa pembeni katika michezo hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa timu hiyo, Philip Alando, alisema mchezaji huyo amekwenda Uganda kwa ajili ya programu maalumu ili aweze kurejea katika hali yake.

“Ngoma huku hajaanza kucheza, ila anafanya mazoezi yake ya Gym na uwanjani ili aweze kuwa fiti zaidi, programu hii ipo kwa kila mchezaji ili awe fiti,” alisema.

Wakati huohuo, mchezaji Yakub Mohammed, ambaye alipata majeraha ya goti tangu mwishoni mwa msimu uliopita, naye hayupo katika kambi hiyo na alionekana jijini Dar es Salaam katika mechi ya Simba na Asante Kotoko.

“Yakub amebaki Tanzania anaendelea na mazoezi kwa kufuata utaratibu wa daktari wake, tukirudi tutaungana naye kwa maandalizi ya Ligi Kuu Bara,” alisema.