Nigeria yafufua matumaini Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Mabao ya Nigeria yalifungwa na Ahmed Musa kipindi cha pili  na kuwafanya Waafrika kurudisha matumaini kwa timu hiyo ambayo ilianza vibaya mchezo wake wa kwanza kwenye kundi hilo.

Timu ya Nigeria imefufua matumaini ya kusonga mbele baada ya kufikisha pointi 3 kwenye kundi D ikiwa nyuma ya vinara Croatia kutokana na ushindi mnono walioupata kwa kuilaza Iceland mabao 2-0.

Mabao ya Nigeria yalifungwa na Ahmed Musa kipindi cha pili  na kuwafanya Waafrika kurudisha matumaini kwa timu hiyo ambayo ilianza vibaya mchezo wake wa kwanza kwenye kundi hilo.

Ushindi huo unaiweka Argentina kwenye wakati mgumu wa kusonga mbele kutokana na kuwa na alama moja mkiani kwenye kundi D.

Timu za Misri na Morroco tayari zimepoteza nafasi ya kusonga mbele hivyo, Senegal na Nigeria zinakuwa timu pekee zilizobeba matumaini ya Waafrika kwa sasa.

Nigeria walianza mchezo huo kwa kasi wakionekana kujiamini kipindi cha kwanza na kipindi cha pili kabla ya kuweka mabao hayo wavuni.

Iceland walikosa penalti ambayo awali mwamuzi aliamuru adhabu kutokana na mchezaji wao kuchezewa vibaya. Hata hivyo penalti hiyo iliota mbaya baada ya kupigwa na kutoka nje.

Kundi D lina timu za Croatia, Nigeria, Iceland na Argentina.

Kikosi cha Nigeri akilichoanza kilikuwa : Uzoho, Omeruo, Troost-Ekong, Balogun, Moses, Etebo, Mikel, Ndidi, Idowu (Ebuehi), Musa, Iheanacho .

Benchi la lilikuwa na nyota; Ezenwa, Echiejile, Ighalo, Abdullahi, Simy, Obi, Onazi, Iwobi, Ogu, Awaziem, Akpeyi.