Ngassa, Makambo wabanwa mapema

KIKOSI cha Yanga kinaendelea na mazoezi kambini mjini Morogoro, lakini katika kuhakikisha nyota wapya na wale wa zamani wanawajibika kwa nidhamu kubwa mabosi wa klabu hiyo wameamua kufumua mikataba yao ili kuwabana zaidi.

Mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania wamesajili wachezaji saba wapya akiwamo Mrisho Ngassa, Deus Kaseke, Heritier Makambo, Nkisi Kindoki Klaus, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Jaffa Mohammed na Mohammed Issa ‘Mo Banka’.

Hata hivyo mabosi wao wamepata akili moja ya kutaka kuwabana wachezaji kwa kuhakikisha nidhamu na uwajibikaji vikitangulia mbele na katika akili hiyo mabosi wa timu hiyo wamefumua mikataba yao na kuweka vipengele vigumu.

Taarifa kutoka Yanga ni kwamba kila mchezaji aliyesaini mkataba katika dirisha lililopita kuna mabadiliko makubwa katika mkataba wake ambapo baadhi ya vipengele vigumu vimeongezwa.

Moja ya vipengele hivyo ni kumtaka kila mchezaji kuwajibika ipasavyo katika kuwania namba ambapo kama uwezo wake utaonekana kushuka anaweza kukosa sehemu ya fedha zake za usajili.

Kitakachofanyika Yanga ni kwamba endapo mchezaji amesaini mkataba wa miaka miwili atapewa nusu ya dau la usajili kisha kiasi kilichosalia atapewa kabla ya kuanza mwaka wa pili.

Utata unakuja kabla ya kufanyiwa malipo hayo tathmini itafanyika juu ya mchezaji husika alivyoitumikia Yanga kwa mwaka wa kwanza na kama itaonekana kiwango chake kimeshuka anaweza kujikuta kiasi hicho kikimegwa au kusitishiwa mikataba.

Katika mikataba iliyopita kipengele kigumu kilikuwa endapo mchezaji atashindwa kucheza mechi kwa asilimia 10 anaweza kuachwa bila kulipwa fedha za usajili akilipwa mshahara wa mwezi mmoja pekee.

Mbali ya kipengele hicho Mwanaspoti linafahamu kwamba kabla ya kuanza ligi kila mchezaji aliyesajiliwa msimu huu na wale waliotumikia Yanga msimu uliopita atakabidhiwa fomu maalum za kusaini kanuni mpya za uwajibikaji katika klabu yao kuzuia hatua za migomo ya mara kwa mara.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaaya, alipotafutwa na Mwanaspoti ili kufafanua juu ya jambo hilo, alikiri ni kweli wamefanya hivyo akisema imelenga kuhakikisha wanaboresha nidhamu kwa wachezaji ambapo ameweka wazi kuwa kutakuwa na suala la kuchukuliana hatua kwa watakaoendesha migomo.

“Mkataba wa mchezaji ni siri ya mwajiri na mwajiriwa siwezi nikaweka wazi kuwa ni kifungu gani kimewafunga, ninachosema tumeboresha nidhamu,” alisema Kaaya.

Katibu huyo aliongeza suala la wachezaji kushindwa kufika mazoezini bila kutoa taarifa kwa viongozi, kwa wachezaji waliosaini mikataba mipya dirisha kubwa la usajili wamelifanyia kazi na wanaamini walichokiamua kitakuwa suluhisho.

Hivi karibuni nyota wa Yanga walisusia mazoezi na kufungwa Gor Mahia ugenini na nyumbani kwa jumla ya mabao 7-2. Waligoma kushinikiza walipwe fedha zao.