Ngassa, Makambo eti wana vitu adimu

KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kambini mjini Morogoro, lakini vitu ambavyo Mrisho Ngassa na Heritier Makambo wamevionyesha vimemfanya Winga Emmnauel Martin kushindwa kujizuia na kusema nyota hao wapya wana vitu adimu vinavyoweza kuleta mabadiliko makubwa Jangwani msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Martin alisema Ngassa na Makambo wameongeza nguvu kwenye kikosi hicho kutokana na ufundi wao mazoezi huko mkoani Morogoro ambako wameweka kambi kujiandaa na mechi dhidi ya MC Alger, Kombe la FA na Ligi Kuu, kitu kinachowafanya waamini kuna mazuri yatajiri Jangwani.

Martin alisema Makambo anaonekana ni fundi wa kuzifumania nyavu na kwamba ana kasi ya ajabu, akidai kuwa akifanya hivyo kwenye ligi inayoanza Agosti 22 basi Yanga itakuwa imepata mtambo wa mabao kama ilivyokuwa kwa Obrey Chirwa.

“Kwa upande wa Ngassa ni mchezaji mzoefu na hajaisha kama watu wanavyomchukulia, nadhani akiwaliza kwenye ligi ndipo watakapompa saluti, naamini wawili hao kwa safu ya mbele watafanya kitu kikubwa,” alisema.

Mbali na hilo alisema wapo fiti kwa ajili ya kuwakabili MC Alger, Agosti 19 na kwamba watapumzika siku tatu kisha wataenda kuvaana na Mtibwa Sugar kwenye mechi ya ligi kuu, ambapo wataanzia ugenini.

“Tumejiandaa kikamilifu, naamini tutafanya vizuri kwani akili zetu kwa sasa zipo imara kwa ajili ya kukabiliana na ushindani wa wapinzani wetu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

“Baada ya mchezo huo tutapumzika siku tatu, kujiandaa na mechi ya ligi kuu na Mtibwa Sugar, hivyo mashabiki wetu watuamini tutafanya vizuri, wasiache kutuunga mkono,”alisema.