Neymar ataka Cavani auzwe PSG

Muktasari:

Nyota huyo wa Brazil anaona haiwezekani kuendelea kuishi na raia huyo wa kimataifa wa Uruguay baada ya kugombea penalti uwanjani na kufokeana naye katika vyumba vya kubadilishia nguo baada ya mchezo dhidi ya Lyon Jumapili ambapo PSG ilishinda mabao 2-0.

PARIS, UFARANSA. NEYMAR ameitaka PSG kumpiga bei straika mwenzake, Edinson Cavani.
Nyota huyo wa Brazil anaona haiwezekani kuendelea kuishi na raia huyo wa kimataifa wa Uruguay baada ya kugombea penalti uwanjani na kufokeana naye katika vyumba vya kubadilishia nguo baada ya mchezo dhidi ya Lyon Jumapili ambapo PSG ilishinda mabao 2-0.
“Neymar ameshawasilisha madai yake kwa Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi kwamba hataweza kushirikiana na Cavani na ametaka straika huyo wa auzwe,” kimesema chanzo ndani ya klabu hiyo.
Mmiliki wa PSG sasa atakuwa na chaguo la kuamua kutokana na uhusiano huo kati ya nyota wake wawili ambapo mmoja amevunja rekodi ya usajili ya dunia na mwingine ni nyota wa muda mrefu kikosini.
Cavani alichukua uamuzi wa kupiga penalti ambayo hata hivyo alikosa lakini Neymar alionekana kuchukizwa kutokana na mchezaji mwenzake huyo kumgomea asipige mkwaju huo.
Wawili hao waliendelea kuonyeshana umwamba hata baada ya filimbi ya mwishona kubidi kutenganishwa na wachezaji wenzao hali iliyoendelea hadi katika vyumba vya kubadilishia nguo.
Inaaminika kishawishi kimojawapo cha Neymar kuhamia katika timu hiyo yenye maskani yake katika mji mkuu wa Ufaransa ni kuwa mchezaji mkubwa baada ya kuishi katika chini ya kivuli cha Lionel Messi alipokuwa Barcelona.
Na kwa klabu hiyo kulipa Pauni 198 milioni kwa staa huyo mwenye umri wa miaka 25, inadhihirisha kuwa anapaswa kuchukuliwa kama silaha ya maangamizi katika timu.
Kwa upande wake naye, Cavani amefanikiwa kuwa shabiki wa Kocha, Unai Emery kutokana na kukitumikia kikosi hicho kwa miaka minne, akitokea Napoli mwaka 2013.
Ikiwa PSG itataka kumfurahisha supastaa wake mpya itapaswa kumuuza Cavani katika dirisha linalofuata la uhamisho au kutafuta mwafaka wa wawili hao.