Neymar apania kuiua Costa Rica

Moscow, Russia. Nyota wa Brazil, Neymar amepania kinouma nouma, unaambiwa. Baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Switzerland, Straika huyo, anajipanga kuimaliza Costa Rica, katika mchezo wao wa pili wa kundi E, utakaopigwa le, kuanzia saa tisa alasiri.
Fowadi huyo wa Paris Saint-Germain, ni mmoja wa nyota waliokuwa na wakati mgumu katika mchezo wa kwanza kutokana na kukamiwa na mabeki wa Switzerland kiasi cha kujikuta akishindwa kuwabeba Selecao, tofauti na ilivyotarajiwa.
Baada ya kushindwa kutokea mazoezini siku ya Jumatatu, kutokana na tatizo la jeraha la kifundo cha mguu, na baadae kutoka katika mazoezi ya Jumanne akichechemea, kulikuwa na hofu kuwa staa huyo atashindwa kucheza mechi ya Ijumaa.
Hata hivyo, hofu hiyo iliyeyuka baada ya nyota huyo, mwenye umri wa miaka 26, kutokea kwenye mazoezi ya Jumatano akiwa na morali ya kuwakabili Costa Rica. Akizungumza na wanahabari baada ya mazoezi hayo, Neymar alisema:
"Natumai tutacheza kwa kiwango cha juu, mnapokuwa bora lazima kuonesha ubora huo uwanjani, nitajitahidi kufanya kila liwezekanalo, kushinda mechi ya kesho. Tunataka kucheza vizuri, tutacheza vizuri, tumeangalia mkanda wa Costa Rica," alisema.
Baada ya kumalizana na Costa Rica, Brazil ambayo inahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi yao ya kusonga mbele, itamaliza ratiba ya mechi za makundi kwa kuwavaa Serbia, iliyosheheni mastaa kibao akiwemo Alexander Kolarov na Nemanja Matic, Jijini Moscow.