Ndugu zake Mbappe wamtaja Wenger kuinasa saini ya chipukizi huyo aliyeteka soko la usajili Ulaya

Muktasari:

  • Staa huyo anawindwa pia na Paris Saint-Germain, lakini Arsenal wanaamini atashinda dili za vigogo wote hao na kuinasa saini ya kinda huyo wa Kifaransa kwenda kuongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo huko Emirates.

LIVERPOOL ofa yao imepigwa chini na kufanya vita ya kumnasa straika wa AS Monaco, Kylian Mbappe kubaki kuwa ya Real Madrid na Arsene Wenger.

Staa huyo anawindwa pia na Paris Saint-Germain, lakini Arsenal wanaamini atashinda dili za vigogo wote hao na kuinasa saini ya kinda huyo wa Kifaransa kwenda kuongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo huko Emirates.

Ripoti kutoka Hispania zinadai kwamba kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amefanya mawasiliano ya siri na Mbappe na kumwaahidi kwamba ile safu yake ya washambuliaji watatu matata, Karim Benzema, Gareth Bale na Cristiano Ronaldo mmoja ataondoka na nafasi yake atakuja kuingia yeye.

Lakini, hilo likiwa likiendelea huko Hispania, huko England Arsenal ina imani kubwa ya kuipata saini ya mchezaji huyo baada ya wenzake Liverpool ofa yao kutupwa huko kwenye 'dastibini' na AS Monaco kwa madai kwamba mchezaji mwenyewe anataka kwenda Santiago Bernabeu.

Taarifa kutoka Ufaransa zinadai ndugu wa mshambuliaji huyo wanaamini kwamba, Mbappe anaweza kuamua kuichagua Arsenal kwa ajili ya kocha Wenger.

Le Parisien lilifanya mahojiano na ndugu wa Mbappe na mmoja wao alisema hivi: "Wenger ni mmoja wa makocha makini sana. Kama Kylian atasaini Arsenal kesho basi ni kwa sababu ya Wenger.

"Anajua jinsi ya kuwatengeneza vijana na kuwa wachezaji bora hasa baada ya kufanya hivyo kwa mastraika wa zamani wa Ufaransa, Thierry Henry na Nicolas Anelka. Kukosa Ligi ya Mabingwa Ulaya? Sidhani kama Europa League inaweza kuwa kikwazo."