Nduda atia matumaini Simba

Muktasari:

  • Kipa huyo alikuwa kipa bora wa mashindano ya Cosafa yaliyofanyika Afrika Kusini mwezi Julai

Dar es Salaam. Kipa wa Simba, Said Mohamed 'Nduda' ameanza kufanya mazoezi mepesi baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti lake.

Nduda amefanyiwa upasuaji wa goti la mguu wa kulia India na tayari amerejea Tanzania kuendelea na programu za mazoezi ili aweze kurejea kwenye majukumu yake.

 "Kwa sasa hali yangu imeanza kuimalika tofauti na awali ambapo nilikuwa napata maumivu makali, nafanya mazoezi mepesi, yatakayonichukua miezi miwili baada ya hapo nitamsikiliza daktari kama naweza kuendelea na timu au kuna programu gani itafuatia," alisema.

Alisema kila hatua ya mazoezi atakayofanywa yanapangwa na daktari kutokana na maendeleo yake na anavyojisikia.

"Nafanyia mazoezi nyumbani ila programu zote nimepewa na daktari, najiona naendelea vema naamini nitarejea katika majukumu yangu baada ya huo muda, natamani kuona natoa mchango ili tuweze kutimiza ndoto yetu ya ubingwa," alisema Nduda.