Ndoa ya Uwoya, Dogo Janja pasua kichwa

Muktasari:

Gumzo hilo lilikuwa moto kutokana na utofauti wa umri uliokuwepo kati ya wawili hao, kwani Uwoya anadai kuwa na miaka 29, wakati Dogo Janja anaelezwa kuwa na miaka 23 tu. Hata hivyo wenyewe wanasema halina shida kwani umri ni namba tu haiingiliani na suala la mapenzi.

IMEPITA miezi mitano sasa tangu, wasanii wawili wa Bongo, Irene Uwoya anayetamba kwenye Filamu na Dogo Janja anayekimbiza kwenye Bongo Fleva kufunga ndoa iliyoleta gumzo kila kona.

Gumzo hilo lilikuwa moto kutokana na utofauti wa umri uliokuwepo kati ya wawili hao, kwani Uwoya anadai kuwa na miaka 29, wakati Dogo Janja anaelezwa kuwa na miaka 23 tu. Hata hivyo wenyewe wanasema halina shida kwani umri ni namba tu haiingiliani na suala la mapenzi.

Pamoja na awali Uwoya kutokuwa huru hasa kuonekana hadharani na Dogo Janja wala kukiri kuhusu ndoa hii, hivi sasa jambo hilo limeonekana kumshinda, kwani amekuwa akifunguka na kutupia mipichapicha kwa raha zake.

Siku ya kwanza wawili hao walionekana pamoja katika harusi ya Msanii Zuwena Mohammed ’Shilole’, na baada ya hapo ikiwa ni meseji za mahaba niue kwenye kurasa zao za Instagram.

Pia mara ya pili kwa wawili hao kudhihirisha kuwa ni mume na mke ni pale walihojiwa kwa wakati mmoja katika kipindi cha Leo Tena, kinachorushwa na kituo cha Redio cha Clouds FM.

Katika mahojiano hayo kila mmoja alionyesha namna gani alivyokolea kwa mwenzake, ambapo Uwoya alidai kwamba anamuamini Dogo kwa asilimia 80 wakati Dogo akisema anamuamini kwa asilimia 100.

Ni kutokana na asilimia hizo 20 zilizobaki katika uaminifu huo, Uwoya alisema amelazimika kumuamuru Dogo katika wimbo wake mpya wa Wayu Wayu, kutopiga picha na wanawake na badala yake akajigeuza na kucheza kama mwanamke.

Alipoulizwa kama itakuwa hivyo kwa nyimbo zote, Uwoya alisema ndio na kueleza kuwa atawatumia hata ndugu zake au wa Dogo kwani katika familia zao kuna wasichana wengi ambao wanaweza kufanya kazi hiyo.

Hata hivyo, wakati wawili hao wakionyesha mahaba niue hadharani, yapo mambo matano ambayo yanaiweka ndoa hiyo matatani.

Mila na Desturi

Kwa mila na desturi za kiafrika ni lazima watu mnapotaka kuoana muende kutambulishana nyumbani kabla ya yote. Huo ni utaratibu wa lazima na hauna makonakona.

Katika hili kwa wale wenye uwezo hufanya mpaka sherehe ambayo hujumuisha kuvalishana pete ya uchumba na ndugu wa pande zote kuhudhuria.

Wengine wamekuwa wakifanyia sherehe hii nyumbani na wengine Kanisani. Kwa Dogo Janja na Uwoya haikuwa hivyo kwani harusi yao imekuwa ya ghafla na kuonekana mtandaoni wakiwa wameshafunga ndoa huku waalikwa wakiwa wachache ambao ni watu wao wa karibu hususani marafiki.

Wakati Uwoya mzazi wake hata mmoja hakuonekana, kwa Dogo Janja bosi wake wa kundi la Tip Top Connections, Madee alisimama kama baba yake na baraka zote za kufanya hivyo zilitoka kwa mama wa msanii huyo anayeishi Jijini Arusha.

Suala la Dini

Wakati mama Uwoya akiikataa ndoa hiyo kwa madai kuwa ni batili, kwa upande wa dini, ndoa hii ni halali na inatambulika ni rasmi kwa mujibu wa dini ya Kiislam kama anavyoelezea Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum aliyewahi kufanya mahojiano na gazeti la Mwananchi Januari mwaka huu.

Katika maelezo Sheikh Alhad anasema ndoa katika dini ya Uislam ni halali hata kama Uwoya hakupewa talaka na mumewe.

Anasema uhalali wa ndoa hiyo unakuja baada ya mwanamke kuhama kutoka kwenye dini yake ya zamani na kujiunga na Uislamu.

Wakati Uislam ukieleza hivyo, kwa upande wa KKKT ambako Uwoya na mumuwe marehemu Ndikumana walifunga ndoa, wanandoa hutenganishwa na kifo.

Hata hivyo kama ikatokea kuna makosa yamefanywa kati ya wawili hao ni lazma waitwe kwenye baraza la usuluhishi na kuwepo na ushahidi wa kinachotaka kiwatenganisha jambo ambalo Uwoya na Ndikumana wazazi wake wanaeleza hawajawahi kulifanya.

Hata hivyo wiki chache baada ya harusi ya Uwoya na Dogo Janja, aliyekuwa mume wa Uwoya, Ndikumana alifariki dunia na kumfanya awe huru kwani kwa KKKT mwanandoa mmoja akifariki, suala la kuamua kuoa au kuolewa hubaki kwa mhusika na dini yao inaruhusu.

Sheria ya Serikali

Kwa upande wa sheria za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndoa ya wasanii hawa pia inatambulika kisheria kama ambavyo Ofisa Usajili Mwandamizi Kitengo cha Ndoa na Talaka, kutoka Wakala wa Msajili , Mfilisi na Udhamini(RITA), Husna Mfundo, anaeleza.

Mfundo anasema katika sheria za ndoa zinazotambuliwa Serikalini, kama mwanamke amebadili dini wanaitambua kisheria kuwa ni halali.

“Ndoa ya aina hii hata kama mwanamke hajapewa talaka, inakubaliwa tofauti na ya kikristo ambayo mpaka wapate ushahidi wa kimahakama ndio mwanamke anaruhusiwa kuolewa na mwanaume mwingine,” anasema.

Pamoja na mkanganyiko huo uliopo, ni wazi kwamba huenda Dogo na Irene walijidhihirisha yote haya kabla ya kuchukua maamuzi ya kufunga ndoa hivyo ili baade isije ikabainika kuwa ni batili.

Kazi ya Sanaa

Jambo jingine ni suala zima la wawili hao kuwa wasanii, kiasi ya kwamba baadhi ya watu bado wanaamini kuwa ndoa hiyo ni ya kuigiza na kutokana na tabia ya baadhi ya wasanii kufanya vitu vya uongo vyenye kuvuta hisia za wengi ili waweze tu kupata kiki mtaani.

Jambo hili hata mama na baba wa Uwoya wamelieleza na kusema kuwa mara ya kwanza walipouuliza waliambiwa ni Filamu na walibaki kuamini hilo kwa kuwa wanamjua mtoto wao ni msanii. Hata hivyo kumbe kitu ni ndani ya boksi.

Familia zao

Wakati wawili hao wakiwa katika mahaba niue, bado familia ya Uwoya haijamkubali Dogo Janja.

Akizungumza na Mwanaspoti, mama wa Uwoya, Neema Mrisho, anasema hadi sasa ndoa hiyo hawaitambui na hampendi Dogo Janja kwa kuwa hana adabu.

“Kama kweli huyo Dogo Janja ana adabu na anajua taratibu za kumposa mtoto wa kike, kwa nini hakuja kwanza nyumbani na badala yake wakaamua kufunga ndoa kama sio kukosa adabu huko?,” anahoji mama huyo.

Hata hivyo anasema kwa upande wa mtoto wao Uwoya, amekuwa muoga kulifanya hilo kwa kuwa anajua wakati wanafunga ndoa hiyo alikuwa na ndoa tayari ya marehemu Hamad Ndikumana ambapo mpaka kufariki walikuwa hawajawahi kutalakiana hivyo isingekuwa rahisi kuwapelekea mwanaume mwingine.

Kauli ya mama huyo inapishana na ya mwanaye Uwoya ambayo alipohojiwa na kituo kimoja cha redio alisema walishaachana na Ndikumana ambaye alikuwa msakata kabumbu na kuamua kuishi na mwanamke mwingine .

Wakati kwa upande wa Dogo Janja anadai kisa cha kushindwa kumpeleka nyumbani kwao ni kutokana na wazazi wake kuwa watu wa safari jambo ambalo mama yake anakanusha na kueleza kwamba hata kama ni kusafiri hawezi kusafiri mwaka mzima na kuongeza kuwa basi tu mtoto wao anaona aibu kwa kitendo alichokifanya na kusisitiza kuwa ndoa hiyo itabaki kutambuliwa na waliomwafungisha na ndugu ambao Uwoya aliwaita ambao wao hawawatambui kwenye ukoo wao.