Ndo mnaishi hivi? Mnaharibu ndoa yenu

Muktasari:

  • Achana na hizi changamoto ndogondogo za kumalizana chumbani kama wana ndoa. Zipo nyingine hazizuiliki na mwisho wake ni kutengana na kuachana kabisa.

KUNA watu wako kwenye ndoa lakini hawajui ni vipi waishi na wenza wao ili kuidunisha ndoa yao. Huo ni ulimbukeni.

Kila aliye kwenye ndoa ajue ana jukumu kubwa la kuhakikisha anaisimamisha ndoa yake na kamwe haivunjiki.

Achana na hizi changamoto ndogondogo za kumalizana chumbani kama wana ndoa. Zipo nyingine hazizuiliki na mwisho wake ni kutengana na kuachana kabisa.

Kama wewe upo kwenye ndoa yako lakini bado ukaendekeza mambo haya, pole sana, ndoa yako utakuwa unaichimbia kaburi mwenyewe na hakuna wa kumlaumu kwani suala la ndoa ni la kuheshimiwa na kujali.

UBINAFSI NDANI YA NDOA

Mambo kama haya ya nini ndani ya ndoa? Tayari mmeshakuwa kitu kimoja, ubinafsi unakujaje.

Kumekuwa na tabia hii hasa kwa wanawake. Ni kweli hata wanaume wengi wamekuwa wakilalamika wanawake wao ni wabinafsi. Wamekuwa na tabia za kuficha pesa zao. Kwa mfano, pesa anazopata kwa mume wake, anaficha kisha anakwenda kujenga kwao.

Ndugu yangu, hayo mambo hayafai. Hata kama ni suala la kujenga, jaribu kumshirikisha mumeo. Kwa nini usimwamini na kumfanya awe mshauri wako. Haya sasa umeenda kujenga kwani akija kujua unadhani kuna ndoa tena hapo. Shauri yako.

NYUMBA NDOGO

Hii ni sana sana kwa wanaume. Mwanaume ameoa kisha anatafuta mwanamke wa nje na anamfanyia kila kitu hata zaidi ya mkewe.

Anamjengea nyumba, kama ni kodi anamlipia na mahitaji mengine yote muhimu ambayo yatamridhisha kwa kujua tu, hata yeye anapata kile atakacho.

Nikuulize wewe mwanamume, uliye naye nyumbani hakutoshi hadi ukimbizane na wanawake wa nje.

KUKASIRIKA

Unakuta siku nzima ndani hakuna anayemwongelesha mwenzake. Kila mtu anaanza kufikiria mengine ikiwezekana kutafuta mpango wa nje. Neno samahani ni neno dogo sana na kama mtalitumia vizuri litaokoa ndoa yenu. Unakuta mume kamsemesha mke wake jambo dogo tu na yeye anaanza kushambulia kwa maneno makali na mwishowe anaishia kununa na kuona anaonewa.

Au unakuta mke amemkumbusha mume wake sehemu ya wajibu wake kama kichwa cha familia, lakini kinachofuata ni kumtupia maneno makali na kuifanya nyumba kutokukalika. Ndugu yangu jua kabisa kama tabia itakuwa hivyo, mwishowe ni kila mtu atatafuta njia yake na kuwa mwisho wa ndoa yenu.

UVUMILIVU

Matatizo ni sehemu ya changamoto za kimaisha. Hayakwepeki na kama hutakuwa makini unaweza ukajikuta unachukua uamuzi mbaya.

Yachukulie matatizo ya mwenzako kama sehemu ya maisha yako na kujua wazi ni yenu wote, lakini kama utaamua kuwa na tabia ya kuona mwenza wako ndiye mwenye matatizo na wewe huna, basi ujue utamshosha mwenzako ambaye anajitahidi kutengeneza mambo wewe unakuwa mwepesi wa kukata tamaa.

Hiyo tabia itakuponza na kuifanya ndoa yako kuwa katika hatari ya kusambaratika. Matatizo ni yenu wote hivyo uvumilivu unatakiwa ili kipindi kigumu kipite na si kuonana wabaya kwamba mmoja wenu ni nuksi.

Mnatakiwa mpigane pamoja na kushinda maisha pamoja na si kulaumiana na mwishowe kuivunja ile nguvu yenu ya pamoja nakujikuta mkitengana kwa mambo ambayo yanavumilika.