Ndemla, Mo Ibra Yanga dili moto

WAKATI beki wa kati wa Kagera Sugar, Juma Said ‘Nyosso’ akichomoa kimtindo kutua Jangwani, dili za viungo mahiri wa Simba, Mohammed ‘MO’ Ibrahim na Said Ndemla kutua Yanga limefikia pazuri, japo Simba wameamua kukomaa nao ili wasalie kikosini.

Yanga imekuwa ikiwataka viungo hao ambao wamekuwa hawana nafasi katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, lakini inasuasua kwa sababu ya masharti magumu yaliyowakwaza.

Hata hivyo inaelezwa kuwa masharti ya wachezaji hao yanaendelea kujadiliwa Yanga ili kuona kama inawezekana watue Jangwani.

Habari za uhakika toka ndani ya Yanga zinasema kuwa Mo Ibrahim na Ndemla wanahitajika kwa udi na uvumba, japo kuna mgawanyiko wa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo na hasa dau wanalolitaka na viwango walivyoonyesha.

Inadaiwa ishu ya Ndemla kwa sasa inajadiliwa, huku dili la Mo Ibrahim likibaki fifte fifte kwa vile Simba imeamua kukomaa naye ili abaki Msimbazi.

Juzi Jumanne Simba walijadiliana na mchezaji huyo ili asaini mkataba mpya wa miaka miwili uliotarajiwa kusainiwa leo Alhamisi, huku ikielezwa asilimia 98 huenda kiungo huyo akasalia Msimbazi.

Meneja wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo ameliambia Mwanaspoti kuwa anaamini mchezaji wake ana uwezo wa kupambana na kupata namba ndani ya Simba na timu yoyote na ndiyo maana mazungumzo yao na viongozi wa Simba ya kumbakiza kwenye kikosi hicho yamekamilika kwa asilimia kubwa, huku akikiri Yanga pia ikimpigia hesabu.

“MO ni mchezaji mwenye akili zake ana uwezo wa kuamua jambo, anajua mahitaji yake ni yapi, tumekubaliana na Simba na uwezekano ni mkubwa wa kusaini mkataba mpya lakini asilimia chache zilizobaki pia zinaweza kuletea mabadiliko kutokana na mchezaji mwenyewe, ila anaweza kubaki Simba, alisema.

Kwa upande wa Mwanasheria wa Ndemla, Kelvin Eric, ameliambia Mwanaspoti kuwa mpango wake wa kwenda Yanga ama timu yoyote inayomhitaji bado unajadiliwa kwani kuna mahitaji muhimu ambayo anapaswa mchezaji apewe.

“Bado kuna muda wa usajili, tunafanya mazungumzo na timu mbalimbali ndani na nje ya nchi, hivyo siwezi kutamka moja kwa moja kuwa Ndemla atacheza wapi msimu ujao, Yanga, Simba na wengine wote bado tunaendelea na mazungumzo. Kuna vitu vingi tunaangalia ambavyo mchezaji anakwenda kuvipata huko anakoenda.

“Wengi wanaangalia pesa pekee, lakini sisi hatuangalia hilo tu, bali kikubwa ambacho pia tunakihitaji mkataba wake ni kuwepo na kipengele cha mchezaji kupata nafasi ya kucheza ingawa hili pia huangaliwa na kocha,” alisema mwanasheria huyo.

“Wachezaji wanasajiliwa kwa pesa ndogo lakini kiwango wanachokiweka mchezaji anapotaka kuondoka ni kikubwa mno, jambo ambalo kisheria siyo sahihi kwani kuvunja mkataba ni haki na mtu sehemu yoyote ile, suala la Ndemla litakamilika na atacheza timu yoyote ambayo tutaafikiana nayo ila siyo kwa haraka namna hii,” alisema Eric.

Nyosso agoma

Katika hatua nyingine beki mkongwe Juma Nyosso aliyekuwa akitajwa kwenye usajili wa Yanga, amesema msimu ujao anabaki kuitumikia Kagera Sugar.

“Hayo ni maneno tu, mimi nimemalizana na viongozi wangu wa Kagera, usajili bado lakini tumekubaliana kuongeza mkataba wa mwaka mmoja,” alisema.