NGOMA AMEPONA GOTI, ATACHEZA WIKI IJAYO?

Muktasari:

Habari hizi zilitolewa siku tatu zilizopita na Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten na kutolewa ufafanuzi na Daktari wa Klabu hiyo, Edward Bavu.

STRAIKA mahiri wa Yanga, Donald Ngoma imeelezwa sasa amepona majeraha ya goti yaliyomfanya kuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitano.

Habari hizi zilitolewa siku tatu zilizopita na Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten na kutolewa ufafanuzi na Daktari wa Klabu hiyo, Edward Bavu.

Walisema tayari Ngoma amepona na amenza mazoezi mepesi binafsi lakini ni mapema mno kucheza mechi za wiki ijayo.

Ngoma alipatwa na majeraha ya goti mwaka jana mwishoni mwa Novemba katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini hakuvunjika bali ni majeraha ya tishu laini za goti .

Swali kubwa ambalo linabaki kichwani mwa mashabiki, je atacheza mechi za wiki ijayo?

Leo nitaeleza zaidi mambo yanayofanyika baada ya kupona majeraha ya tishu laini za ungio la goti na kufahamu kama ni sahihi kwa mwanasoka kurejea uwanjani na kucheza mara tu maumivu yanapoisha.

MAMBO HUANZA HIVI

Ukiacha majeraha ya kuvunjika mifupa inayounda goti yanayoweza kuchukua wiki 6-12 kuunga na kupona kabisa, nyuzi zinazoshikilia mifupa hiyo zikipata majeraha makubwa yanaweza yasipone kwa wakati. Kuna uwezekano mkubwa jeraha alilopata lilikuwa ni kukatika kwa nyuzi kubwa mojawapo inayoshikilia goti pamoja na tishu za jirani na goti, ambazo huchukua muda kupona. Nyuzi hizi hujulikana kitabibu kama ligaments, kazi zake ni kuunganisha mfupa mmoja na mwingine ili kuunda ungio (joint) na katika goti ziko nne.

Nyuzi ya mbele ijulikanayo kama Anterior Crusate Ligament (ACL) iliyo na umbile kama herufi “X” ndiyo inayokumbwa na majeraha makubwa kwa wachezaji wa soka. Ukubwa wa majeraha haya yanaweza kuainishwa katika makundi matatu, majeraha ya kawaida, ya kati na makubwa.

Nyuzi hizo zinazoshikilia zinaweza kujeruhiwa na kuvutika kupita kiwango, kuchanika kidogo, kuchanika na kuachana pande mbili au kukwanyuka kutoka katika mfupa uliojipachika. Pale inapokatika pande mbili au kukwanyuka na kutoka katika mfupa uliojipachika, mejeraha ya aina hii ndiyo makubwa kwa goti na huchukua muda mrefu kupona.

Inaweza pia ikatokea ukapona na kuhisi maumivu yameisha kabisa kumbe kwa ndani bado.

Goti ni mojawapo ya ungio (joint) ambalo kwa mwanasoka ni eneo ambalo lipo katika hatari ya kujeruhiwa zaidi kuliko maungio mengine kutokana na kubebea shinikizo kubwa la uzito wa mwili na huku mchezo wenyewe ukihitaji goti kufanya kazi wakati wa kucheza. Goti ni aina ya ungio bawawa lenye mijongeo mikuu mitatu ikiwamo kunyooka, kujikunja na kujizungusha.

Kukaa nje ya uwanja kwa miezi mitano ni muda mzuri wa kutosha kupumzika na ni nafasi nzuri kwa mchezaji kupona endapo tu bainisho la jeraha lake (diognosis) na matibabu yalikuwa sahihi. Vile vile, kama mchezaji alikuwa anashikamana na matibabu na ushauri anaopewa ni jambo la msingi kupona kwa wakati.

Kupona kwa majeraha pia hutegemea vitu kama kinga ya mwili ya mchezaji, lishe, ukubwa na aina ya jeraha, eneo lilipo jeraha, umri wa mchezaji, mwili kuoana na matibabu, matumizi ya dawa za maumivu kiholela na kuongezeka uzito wa mwili kupita kiwango. Vile vile kama mchezaji atakuwa na mwenendo mbaya kimaisha ikiwamo unywaji pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara, matumizi ya vilevi vingine, kutopata mapumziko na msongo wa mawazo.

Haya ndiyo mambo ambayo yanatoa mstakabali wa kupona jeraha kwa wakati na huku mchezaji akirudi uwanjani akiwa imara kiafya na kiwango chake kikiwa kile kile alichokuwa nacho awali.

Mchezaji asipopona vizuri au akawa hana maumivu lakini kumbe jeraha kwa ndani halijapona hatari ya kujeruhiwa tena huwa ni kubwa na vile vile akiwa hajapona vizuri hawezi kucheza kwa kiwango cha juu.

Ni kawaida pia kwa mchezaji kuathirika kiakili, kutokana na kumbukumbua ya jeraha alilopata kumnasa kichwani mwake hujikuta anakuwa mwoga kucheza kwa uhuru hivyo kuathiri kiwango chake.

Mfano kwa hatua ambayo amefikia Ngoma ambaye kwa sasa hana maumivu na ameanza kujifua kwa mazoezi mepesi akiwa mwenyewe, jambo hili kitabibu ni sahihi kabisa.

Kwa mchezaji anayetoka majeraha, kama daktari wa timu na amethibitisha kuwa amepona na hana maumivu hatua zinazofuata sasa ndiyo kama hizo zinazofanyika kwa Ngoma. Huwezi kuamua ghafla tu mchezaji aliyekuwa majeruhi na sasa kupona na hana maumivu ukamuingiza kucheza mechi zenye ushindani.

Kwa kawaida mchezaji anapochunguzwa kuwa amepona na hana maumivu tena na wataalam wa afya wakathibitisha hilo, mambo yanayofuata huwa ni kama ifuatavyo.

Mchezaji huyo ataanzishiwa mazoezi maalum ya viungo ikiwamo mazoezi mepesi ya kunyoosha na kulainisha viungo vya mwili, mazoezi ya kupasha mwili moto na mazoezi ya kuimarisha viungo. Atafanyiwa majaribio mbalimbali ikiwamo utimamu wa kimwili kiujumla, kupima kasi katika mbio fupi fupi na ndefu.

Vile vile atafanyiwa jaribio la ufanyaji wa maamuzi ya haraka uwanjani, matumizi ya ujuzi wake uwanjani na namna viungo vya mwili unavyoshirikiana na ubongo kutenda vitendo (coordination), ndipo ataanza taratibu huchanganywa na wenzake na kufanya mazoezi ya pamoja.

Katika hatua za kuanza kumchezesha anaweza kuchezeshwa katika mazoezi ya timu, akaingizwa kuchezeshwa dakika 15 siku ya kwanza, siku ya pili 30 na siku ya tatu 45.

Tathimini ikifanyika wakabaini hana tatizo lolote na kiwango kina ridhisha basi baadaye katika mazoezi anaweza kucheza dakika 90 kwa siku kadhaa (siku 3-7 mfululizo au kwa muachano wa siku). Baadaye anaweza kuingizwa katika mechi za ligi kwa tahadhari, anaweza kuingizwa mechi zisizo na ushindani mkali dakika za mwisho za mchezo au mwanzoni mwa mchezo na kutolewa.