NDIO! Ali Kiba a.k.a Mr Musical Genius

Muktasari:

  • Baada ya tafsiri hiyo, nikulete kwenye maandishi ya mchambuzi wa muziki wa Forbes, Ian Morris, katika uchambuzi wake uliochapishwa Novemba 17, 2014 aliandika: “Technology is Destroying The Music Industry” akimaanisha teknolojia inaharibu tasnia ya muziki.

Nianze na tafsiri ‘Musical Genius’ ni mtu mwenye mawazo mengi na bora ya kimuziki. Iwe halisi au kwa kutafsiri na kuendeleza kilichoanzishwa na wengine. Muhimu zaidi ni kuwa Musical Genius ni mtu mwenye uwezo mkubwa kuiwasilisha sanaa kwa kiwango kilichosheheni ufundi.

Baada ya tafsiri hiyo, nikulete kwenye maandishi ya mchambuzi wa muziki wa Forbes, Ian Morris, katika uchambuzi wake uliochapishwa Novemba 17, 2014 aliandika: “Technology is Destroying The Music Industry” akimaanisha teknolojia inaharibu tasnia ya muziki.

Mdogo mdogo tutaelewana; naendelea. Novemba 30, 2017, memba wa zamani wa Bendi ya Gay Daddy ya Uingereza, Cliff Jones alitoa mtazamo namna jamii ya muziki wa studio inavyoharibu mantiki kamili ya muziki.

Alichokisema Morris kina msingi mmoja kuwa siku hizi teknolojia imerahisisha mno upatikanaji wa fedha, kiasi kwamba njia za mkato ni nyingi kuupeleka wimbo sokoni. Hivyo, mwanamuziki anaweza kufanya kazi mbaya lakini akaipeleka YouTube, ikiwa na vitu vya kuvutia watu, itatazamwa na kupendwa.

Vitu hivyo vya kuvutia watu vinaweza kuwa si vya kimuziki. Kwa maana mtu anafanya muziki katika ubora mdogo, ama kwa kupungukiwa utaalamu au kurahisisha mchakato ili kuwahi soko. Hata hivyo, video inakuwa na vitu vyenye kushawishi kutazama, kwa hiyo inapata watazamaji wengi na fedha inaingia.

Kwa kifupi ni kuwa teknolojia imefanya pesa iwe jirani zaidi. Hatari ya hilo ni kwa watu wengine kutumia mwanya huo kutengeneza vitu kwa haraka haraka, lengo likiwa kuziwahi pesa. Na kwa vile zinapatikana, basi wanafanya mazoea.

Hivyo, Morris anatupa jibu kuwa teknolojia inafanya wanamuziki wakimbilie zaidi pesa. Nyakati za mauzo ya nakala zenye kubebwa mkononi (Hard Copies) zinapitwa. Siku hizi kila mmoja anajitengenezea soko mtandaoni.

UNAJUA HATARI

ILIYOPO?

Hatari inaonekana kwenye ubunifu. Na hapa sasa ni kuungana na Cliff Jones kuhusu muziki wa studio. Teknolojia iliwezesha mtu kwenda studio na kukutana na mtayarishaji (jumla watu wawili), kisha kufanya wimbo mmoja na kuwa mkubwa. Matokeo ya hilo ni bendi kupungukiwa watu.

Kama mwanamuziki na mtayarishaji wake wanaweza kufanya kazi yenye kuwalipa fedha nyingi, kwa nini kufungamana na kundi la watu 30 kufanya bendi moja ambayo malipo yake hutakiwa kugawana? Matokeo ya hilo ni kupungua kwa utunzi, ladha na ubunifu. Kazi ya wengi hujaa ufundi halisi.

Tunaweza kukubaliana sasa kuwa teknolojia ya studio iliua bendi. Maana vifaa vya kwenye bendi vimerahisishwa kiteknolojia.

Sasa ndani ya studio vifaa vinaweza kucharazwa kama ‘live band’, wakati ni mashine tu. Zaidi, teknolojia imerahisha fedha, kwa hiyo watu wana pupa mno kwenye kutengeneza fedha.

Profesa Ken Kragen ni alama ya muziki duniani. Ni mtaalamu wa muziki, vilevile amepata kuwa meneja wa wanamuziki wakubwa kama Lionel Richie, Ken Rogers, The Bee Gees na wengine. Kragen pia ndiye alisimamia mradi wa wimbo “We Are The World”, uliowashirikisha Michael Jackson, Stevie Wonder na kadhalika.

Kragen ni mwalimu wa muziki na katika hilo, ameanzisha darasa linaloitwa Stardom Strategies for Musicians ambalo pamoja na kutoa elimu, hulitumia kuwakutanisha wanafunzi wake na wanamuziki wakubwa ili kupata ujenzi wa kiuzoefu na utaalamu kwa jumla.

Januari 30, 2013, Kragen aliwakutanisha Richie na mtayarishaji mkongwe Marekani, Quincy Jones katika darasa lake.

Na alipokuwa akitoa mada kuhusu jinsi ya kupokelewa sokoni, Kragen alisema: “You can’t sell anything to anybody, whether it’s a song, a script, a product or yourself, until you get their attention.”

Tafsiri yangu: “Huwezi kuuza chochote kwa mtu yeyote, iwe wimbo, muswada, bidhaa au wewe mwenyewe, mpaka upate kugusa hisia zao.”

Sasa tumwelewe Ali Kiba

Maneno ya Prof Kragen yanampambanua Ali Kiba kwamba, anayaishi mafundisho hayo. Amekuwa na utulivu wa hali ya juu katika kuachia nyimbo. Anahakikisha anawatengenezea hamu mashabiki wake na anapotoa wimbo mpya huwa sawa na maji kwa mwenye kiu.

Hivyo si mshangao kuona Kiba akitoa wimbo unakuwa gumzo. Ni kwa sababu anatoa nafasi pana kwa mashabiki wake kutamani kumpokea upya. Tangu Agosti mwaka jana alipotoa Seduce Me, takriban miezi tisa imepita ndipo ameachia kazi mpya. Wimbo unaitwa Moto wa Radi.

Ni vigumu kwa wanamuziki wenye utamaduni wa kuachia wimbo kila baada ya miezi miwili kupata mapokeo kama ya Kiba, maana hawatengenezi hamu ya kupokelewa. Utaratibu wao wa kazi unasababisha wazoeleke na kwa sababu wanaachia ngoma mara kwa mara na ubunifu pia unapungua.

Nakuuliza swali; mwanamuziki ametoa nyimbo tatu ndani ndani ya miezi mitatu, akitoa mpya na yule ambaye alinyamaza mwaka mzima akiachia kazi mpya, nani atavuta hisia zako? Utajiongopea mno kama utasema utamkimbilia aliyetoa nyimbo nyingi mfululizo.

Ujiniaz wa Ali Kiba

Baada ya kukubaliana kuwa Kiba amekuwa na nidhamu ya kuwapa hamu mashabiki wake kuhusu ujio wake mpya, sasa nakuongezea kuwa kikubwa zaidi kinachombeba ni maarifa mengi ya kimuziki aliyonayo. Kiba hazoeleki.

Unaweza kukaa kimya muda mrefu, lakini ukiibuka unatoa wimbo ambao hauna tofauti kubwa na uliopita. Ukifanya mara tatu, taratibu utapoteza nguvu ya kuwajengea hamu mashabiki. Watasema unakaa kimya muda mrefu, lakini ukitoa wimbo ni yaleyale.

Musical Genius ndani ya Kiba ni jinsi ambavyo akitoka leo na kazi mpya, watu hawawezi kutabiri atarudi vipi tena. Kama alivyowaduwaza kwa Aje baada ya Mwana na Chekecha, ndivyo akawaacha taabani na Seduce Me. Sasa ni wa Mvumo wa Radi.

Ukisikiliza Mvumo wa Radi na kubaini sanaa kubwa ndani yake, unajiridhisha kuwa pamoja na ukweli kuwa Kiba anafanya muziki wa studio, hata hivyo, yeye na mtayarishaji wake, Man Water wamekuwa na utulivu katika kubuni vionjo vya kimuziki ambavyo vinafanya anakuwa wa tofauti kila anapotoka upya.

Ukisikiliza nyimbo za Kiba, utaona kuwa si mzuri sana wa kuandika mashairi na wigo wake wa kutoa ujumbe (topic) si mpana kihivyo.

Hata hivyo, Kiba analipa mno kwenye utunzi wa nyimbo, sauti na uwezo wake wa kutambaa bila presha kwenye ala tofauti.

Topic ya wimbo Chekecha ni sawa tu na Mvumo wa Radi, Kiba akimuimbia mpenzi wake kwa ahadi za kumpenda na kumpa thamani kimapenzi. Ila tofauti kubwa ipo kwenye mpangilio wa muziki na mashairi.

Mwisho unapata nyimbo mbili tofauti utadhani zimeimbwa na wanamuziki wawili kila mmoja na wake.

Hiyo ni sababu tosha kwamba, hutakosea ukisema Kiba ataendelea kuwepo sana kwenye soko la muziki.

Ujiniaz wake upo kwenye utulivu, hatoi nyimbo mara kwa mara, hivyo kujenga hamu kubwa kwa mashabiki.

Na akitoa unakuwa wa tofauti mno, hivyo hatabiriki.

Hata sasa, wanajiuliza; baada ya Mvumo wa Radi atarudi vipi safari nyingine?