Mzuka wa Messi na safari ya Amanda Ligi Kuu Marekani

BINADAMU ni viumbe kama walivyo viumbe wengine. Wanazaliwa na kukua. Wanapiga hatua ya maisha japo kila mmoja na njia yake. Hata hivyo, mwishowe wote tuko safarini.

Kila safari moja huanzisha nyingine. Wapo wanaofanikiwa na wengine hujikuta wakichemka. Wapo wanaopitia changamoto nyingi sana kufikia mafanikio na wapo wale wa ganda la ndizi. Wanateleza tu. Hata hivyo, kila kitu na wakati wake.

Hata katika soka, zipo changamoto wachezaji hupitia kabla hujawaona wakiwa nyota duniani. Imetokea kwamastaa wengi wakubwa duniani, waliopita na wanaotamba sasa.

Lionel Messi ni mmoja wao. Ni nyota katika soka, hakuna asiyemjua na kama humjui, tuseme tu uko sayari yako nyingine, sio hapa duniani.

Messi alianza soka akiwa nchini kwao Argentina katika timu ya Newell’s Old Boys ya watoto kabla ya kuchukuliwa na Barcelona ya Hispania na kujiunga na akademia yao ya La Masia alikolelewa kwa miaka kadhaa na kupandishwa kucheza kikosi B na baadae kucheza sambamba na nyota wakubwa katika soka wa kipindi hicho, Ronaldihno Gaucho na Samwel Eto’o.

Messi alipitia kipindi kigumu hadi kufikia mafanikio hayo na kuwa staa mkubwa akizoa tuzo tano tano za mchezaji bora wa dunia, ‘Ballon d’Or’ sawa na mpinzani wake Cristiano Ronaldo aliyetua Juventus hivi karibuni. Hayo ni mafanikio makubwa katika soka.

Alikuwa akianzia benchi kwenye kikosi cha Kocha Frank Rijkaard, huku akimtazama Ronaldinho akifanya vitu vyake na kusubiri huruma ya kocha ili aingie akachukue nafasi ya mtu. Kwa sasa ni mfalme pale Barcelona.

Simulizi ya Messi ni ndefu, hata hivyo, haina tofauti naya kiungo wa Kitanzania, Gloire Amanda anayekipiga Lane United ya Canada.

Amanda anadai anapitia msoto sawa na Messi kwani anakumbana na changamoto nyingi kwenye soka.

Aliitosa Vancouver Whitecaps FC

Vancouver Whitecaps FC ya Ligi Kuu ya Canada ni timu aliyowahi kuichezea nyota wa Singida United Nizar Khalfan miaka ya nyuma. Hata hivyo, hakudumu nayo muda mrefu na kuamua kurejea nchini na kuendelea na soka lake mwaka 2011.

Amanda ambaye alikuwa na kikosi hicho tangu mwaka 2014 ameondoka mwaka jana kutokana na changamoto ya namba na kuhamia kwengine baada ya mkataba wake kumalizika.

“Mambo hayakwenda vizuri nikiwa kikosi B cha Vancouver, nilikichezea hadi mwaka jana na baada ya hapo mkataba wangu ulipomalizika nikaamua kujiunga na Oregon State.

“Lengo la kujiunga na Oregon State, lilikuwa ni kutafuta nafasi ya kutosha ya kucheza soka la ushindani maana nilikuwa Vancouver tangu 2014, lakini niliishia kucheza ligi za kawaida bila ya kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu na mashindano mengine makubwa,” anasema.

Ajipanga pia kielimu

Mbali na kukimbia msoto wa namba pale Vancouver, kiungo huyo mwenye uwezo pia wa kucheza kama mshambuliaji anasema kingine kilichomfanya kuondoka ni kuhitaji kujiendeleza kielimu.

Anasema akiwa na Oregon State, alipata muda wa kutosha kuendelea na chuo. Hata hivyo, baadaye aliomba kwenda kwa mkopo Lane United inayoshiriki Ligi Daraja Nne nchini humo na baada ya kutumika kwa mkopo, Lane United iliamua kumsajili moja kwa moja kabla ya kuomba tena arudi Oregon State kumalizia chuo.

ANUKIA KUCHEZA MLS

MLS ni Ligi Kuu ya Marekani na Amanda anasema anachosubiri kwa sasa ni kumaliza mkataba wake na Lane United iliaamue timu gani akachezee huko,

“Naamini mwakani kama Mungu ataniweka hai utakuwa mwaka wangu, nitatangaza timu nitakayojiunga nayo,” anasema Amanda.

Historia yake

Amanda alizaliwa Novemba 11, 1998, Tanzania kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo mkoani Kigoma.

Akiwa miaka minane tu, familia yake ilihamia Edmonton, Alberta, Canada na huku ndiko alikoanza kujihusisha na soka mwaka 2009 kwenye akademi ya Edmonton Xtreme iliyokuwa karibu na nyumbani.

Mwaka 2012 ndipo kipaji chake kilianza kuonekana na kupata nafasi ya kujiunga na Edmonton Internazionale na baadaye akaichezea, FC Edmonton.

Alisaini mkataba wake wa kwanza wa kucheza soka la kulipwa Machi 31, 2017 akiwa na umri wa miaka 15 kwenye akademi ya Whitecaps ambayo aliitumikia katika mashindano ya kutafuta bingwa wa Canada kwa vijana ‘Canadian Championship’.