Mzuka wa Kichuya Haruna anasubiri

Friday August 11 2017

 

By DORIS MALIYAGA

MASHABIKI wa Simba wamekoshwa na mzuka wa kiungo mpya Haruna Niyonzima. Lakini Kocha Joseph Omog amesema wazi kwamba mpaka sasa anakoshwa na aina ya upambanaji wa Erasto Nyoni na Shiza Kichuya.

Omog alisema: “Nina wachezaji wenye majina makubwa kwenye ligi na walifanya vizuri, lakini ndani ya Simba yangu sitaangalia ukubwa wa majina, nitawapa nafasi wale watakaokuwa na moyo wa kujituma na hamu ya ushindi.

“Kila mchezaji moyoni mwake atambue anatakiwa kupambana,  (Huku anapiga ngumi kwa mikono yote miwili) muda wote, kama tukishinda siyo mabao mawili matatu watu wanaridhika, kama ni kufunga tunatakiwa kufunga mengi tu,”alisema Omog ambaye upo uwezekano akamkosa, Kichuya ambaye anatakiwa na klabu moja nchini Misri.

“Mpaka sasa hali siyo mbaya wachezaji wanajituma kwa nafasi yao, watu kama Kichuya na Nyoni ndiyo mfano mzuri wa aina ya kupambana ninayoimaanisha.”

Kikosi cha Simba kina wachezaji wenye majina makubwa waliofanya vizuri katika misimu ya ligi iliyopita kama, Emmanuel Okwi raia wa Uganda, Mnyarwanda Haruna Niyonzima, John Bocco ‘Adebayor’, Shomari Kapombe,  Nyoni na Aishi Manula.

Wekundu hao ambao ni mabingwa wa Kombe la FA na washindi wa pili wa ligi, wamefanya usajili kuona wanafanya vizuri katika michuano mbalimbali ikiwemo ya kimataifa. Wataiwakilisha nchi kucheza  Kombe la Shirikisho pamoja na Ligi Kuu.

Bado, Omog anahangaika kuhakikisha kikosi kinacheza kwa maelewano yaani kombinesheni: “Kitu kingine, unaweza kuwa na wachezaji wazuri, lakini uchezaji ni kitu kingine, hilo ndiyo nahangaikia kwa sasa, kidogo hali inaanza kuwa sawa, lakini tunachotakiwa ni kucheza mechi nyingi za kirafiki ili wazoeane.”

“Ukiangalia safu ya ulinzi, kati na mbele mwanga upo ingawa pale mbele kuna vitu natakiwa kuvifanya ndani ya kipindi hiki cha maandalizi,”alisema Omog.

ATAKA WINGA  ANAYEINGIA NDANI

Omog, ambaye katika safu ya ushambuliaji anawatumia zaidi, Okwi na Bocco na mawinga, Kichuya pamoja na Mohamed Ibrahim ‘Mo’, amesema: “Kuna kitu nahitaji kwenye safu ya ushambuliaji, nahitaji winga ambaye anaweza kulazimisha kuingia ndani.”

“Nimekuwa nikimtumia Kichuya si mbaya lakini nahitaji mwingine wa namna hiyo au mzuri  zaidi yake,”alisema Omog ambaye anatumia mifumo miwili ya 4-4-2 na 4-3-3.