Nyota Chelsea wamchoka Conte kisa mazoezi

Muktasari:

  • Conte aliiongoza Chelsea kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita

Hali si shwari tena ndani ya Stamford Bridge. Habari ndiyo kama hivyo ulivyosikia, kwamba wachezaji nyota wa Chelsea wamechoshwa na kocha wao Antonio Conte kutokana na kuwafanyika mazoezi yaliyopitiliza kipimo.

Ripoti zinadai kwamba Conte amewazidishia dozi ya mazoezi wachezaji wake na kuwafanya kuwa wachovu wanapokwenda kwenye mechi na hivyo kusababisha tatizo la majeruhi kuwa wengi katika kikosi hicho cha huko London.

Chelsea wapo kwenye ligi msimu huu wakijaribu kutetea ubingwa wao, lakini hadi sasa kwenye Ligi Kuu England zikiwa zimechezwa mechi nane kwa kila timu, wamekusanya pointi 13 tu, wakichapwa mara tatu, sare moja na kushinda mechi nne tu zinazowafanya washike nafasi ya tano, lakini wakiwa wameachwa kwa pointi tisa na vinara Manchester City.

Uchovu huo wa kuwazidishia mazoezi umedaiwa ndicho kisa cha kufungwa mechi mbili mfululizo kwenye Ligi Kuu England na kutoka sare ya 3-3 na AS Roma kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya wao kuanza kuongoza kwa mabao mawili.

 Conte amedaiwa kupunguza siku za mapumziko tofauti na msimu uliopita, ambapo pamoja na kufany mazoezi makali, lakini wachezaji walikuwa wakipata muda mwingi wa kupumzika.

 Hata hivyo, Chelsea msimu uliopita haikuwa na michuano mingi tofauti na msimu huu ambapo inakabiliwa na michuano minne mikubwa, Kombe la Ligi, Kombe la FA, Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya.