Mziba aing’ata sikio Yanga Moro

Muktasari:

  • Aliichambua safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwamba hajaona sababu ya kumrejesha Mrisho Ngassa badala yake wangetafuta vijana ambao wana hamu ya kuvaa jezi hiyo anaamini wangefanya makubwa zaidi.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Abel Mziba ni kati ya mastaa nchini ambao wameacha alama ya kukumbukwa kwenye kikosi cha Yanga na Taifa Stars, kutokana na kazi aliyoifanya uwanjani, amekitazama kikosi cha Wanajangwani cha sasa ameyaona mapungufu na kuwataka viongozi wajiandae kufanya mabadiliko dirisha dogo.
Aliichambua safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwamba hajaona sababu ya kumrejesha Mrisho Ngassa badala yake wangetafuta vijana ambao wana hamu ya kuvaa jezi hiyo anaamini wangefanya makubwa zaidi.
"Siongelei kishabiki, naangalia hadhi ya klabu ya Yanga na kile ambacho wanachopaswa kukivuna uwanjani, kiukweli sioni kama Ngassa peke yake anatosheleza, binafsi naona kuna vijana wengi ambao wanasaka nafasi ya kuichezea timu yetu, hao wangepewa nafasi wangetaka kujitangaza kwa hiyo wangefanya kazi kwa bidii," alisema.
Alimgeukia Heritier Makambo kwamba anatakiwa kutambua nafasi yake inahitaji matokeo na sio kuwepo kwenye timu bila faida, huku akimtaka aangalie rekodi ya mastaa ambao walikuwepo na kutikisa nyavu kama Obrey Chirwa.
"Yanga ina mapungufu katika safu ya mbele na kiungo, ambayo inatakiwa kufanyiwa marekebisho dirisha dogo la usajili, ili tuweze kutwaa ubingwa msimu wa 2018/19, bado namsisitiza Makambo ajue nafasi yake lazima awashawishi watu kwa kufunga na sio kumsifia kwenye mechi ya kirafiki ambayo wamecheza na Mawenzi,"alisema.