Mzee Majuto arejea kutoka India, atangaza kuacha kuigiza

Muktasari:

  • Mzee Majuto alienda India kutibiwa  tezi dume baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu, hata hivyo baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam amepelekwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kupumzishwa kutokana na uchovu wa safari.

Muigizaji na mchekeshaji wa siku nyingi, Amri Athuman maarufu Mzee Majuto leo Ijumaa amewasili kutoka India baada ya kwenda kutibiwa katika Hospital ya Apollo iliyopo jiji la New Delhi.
Mzee Majuto alienda India kutibiwa  tezi dume baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu, hata hivyo baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam amepelekwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kupumzishwa kutokana na uchovu wa safari.
Akizungumza na MCL Digital, Majuto amesema anaendelea  vizuri, anamshukuru Mungu pamoja na Rais John Magufuli kwa kuwezesha matibabu yake yote akiwa nchini India pamoja na Watanzania waliohusika kumuombea.
Mbali na hayo, Majuto amesema akipona ataachana na kuigiza kwani kwa jinsi alivyoteseka hana hamu ya kuigiza ili apate muda mwingi wa kupumzika.
“Nashukuru afya yangu inaendelea vizuri, namshukuru Rais Magufuli kwa kuwezasha safari yangu na matibabu ya kwenda kutibiwa India.
“Pia nawashukuru Watanzania wote kwa maombi yao, nawapenda sana ila naomba wazidi kuniombe ili nipone haraka na jambo langu la kuwaaambia nikipona mimi naacha kuigiza,” alisema Majuto.
Mei 4 mwaka huu alisafirishwa kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu baada ya kuugua kwa takribani miezi mitatu.