Mzee Majuto: Nikifa mtajua tu jamani mimi bado nadunda!

Muktasari:

Mzee Majuto anatoa maneno haya baada ya kusambaa taarifa kwamba amefariki na kutoa wasiwasi Watanzania kuwa yeye ni mzima, kupitia video ambayo amerekodiwa na mkewe Aisha Yusufu akiwa hospitalini.

MUIGIZAJI na mchekeshaji maarufu nchini, Amri Athumani ‘Mzee Majuto’, amesema kama amekufa Yesu Kristo, Mtume Mohammad(SAW) na wazazi wake kwani yeye nani hadi asife na akasisitiza hana wasiwasi na jambo hilo pale muda wake utakapofika.

Mzee Majuto anatoa maneno haya baada ya kusambaa taarifa kwamba amefariki na kutoa wasiwasi Watanzania kuwa yeye ni mzima, kupitia video ambayo amerekodiwa na mkewe Aisha Yusufu akiwa hospitalini.

Muigizaji huyo kwa sasa yupo katika hospitali ya Tumaini akiwa anapatiwa matibabu baada ya kutokea tatizo katika kidonda alichofanyiwa upasuaji wa henia Julai mwaka jana.

Mbali ya henia, pia alishafanyiwa upasuaji wa tezi dume Januari mwaka huu katika hospitali hiyo ya Tumaini na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Hata hivyo akiwa bado anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo, kumezuka taarifa kuanzia jana usiku kwamba  amefariki na hivyo kulazimika kujitokeza hadharani ili kuondoa sintofahamu hiyo.

“Ndugu zangu watanzania mimi ni mzima wa afya, huo uzushi kwamba mimi nimekufa nishauzoea, na hata kama ikatokea nikifa mtapata taarifa tu kwamba nimekufa. Pia sina wasiwasi kwenye kufa, kwani baba na mama yangu  leo hii wako wapi? "anahoji Mzee Majuto na kuongeza.

"Mtume wangu Mohammad yuko wapi, Yesu Kristo yupo wapi na kila mtu anayekula ugali na kwenda chooni  anapaswa kujua kwamba safari ya kufa ipo.”

Mzee Majuto amewahi kutesa na filamu mbalimbali ikiwemo  Welcome Back, Mshamba, Pedeshee, Sio Sawa, Mama Ntilie, Nahama, Gumzo, Mrithi Wangu, Rent House, Ndoa ya Utata, Daladala na Nimekuchoka.

Muigizaji huyu ndiye wa kwanza kuandaa kazi zake katika mikanda na kuuza akiwa na Tanzania Film Company ( TFC) na ameshapata tuzo mbalimbali ikiwemo ya mchekeshaji bora.