Mzambia Simba apewa saa 24

Thursday December 7 2017

 

By THOBIAS SEBASTIAN

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba wanaendelea kupiga tizi la maana kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Dar es Salaam, huku benchi la ufundi la timu hiyo  likiendelea kumsoma Mzambia wao, Jonas Sakuhawa kabla ya kumpa mkataba.

Mzambia huyo kutoka Zesco amepewa saa 24 tu kuanzia sasa ili kuwathibitishia mabosi wa Simba kuwa soka analijua, wakati timu hiyo itakapovaana na KMC iliyopo Ligi Daraja la Kwanza katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu kesho Ijumaa.

Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma anayesimamia mazoezi hayo kwa sasa, alisema Mzambia huyo ambaye Mwanaspoti lilikuwa la kwanza kumripoti kutua

Msimbazi akitokea Zesco ana dakika 90 tu za mchezo huo ili aweze kupewa mkataba.

Djuma alisema Sakuhawa ni mchezaji mzuri na mwenye uzoefu na ameonesha kitu cha ziada tangu walipoanza mazoezi Jumatatu ya wiki hii, japo mazoezi yanahusisha wachezaji wachache kwa sasa, ila ana dakika za kuthibitisha ubora.

“Nitamuangalia vizuri Sakuhawa katika mechi ya Ijumaa (kesho) dhidi ya KMC katika uwanja mzuri wa Azam Complex, kama atatuthibitishia ubora wake uwanjani, anaweza kutusaidia Simba katika eneo la ushambuliaji,” alisema Djuma.

“Tathmini  niliyoifanya mpaka sasa ni kwamba Mzambia huyu ana uzoefu wa kutosha kwani anaonekana amecheza soka kwa muda mrefu, mtulivu na yupo makini lakini nitaona mengine zaidi katika dakika 90 hizo 90 za mechi ya KMC.”

Uwanja  kimeo

Mzambia huyo aliyewahi kucheza TP Mazembe, Lorient ya Ufaransa na El Merreikh ya Sudan, akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya mazoezi ya jana alisema amekuja katika timu kubwa Afrika kwani alikuwa akiisikia Simba kabla ya kutua hapa nchini, ila changamoto aliyokutana naye ni uwanja wa mazoezi.

“Uwanja haupo vizuri zaidi katika eneo la kucheza, ni tofauti na nilipotokea ila nitajitahidi kuonyesha kile ambacho ninacho kwa siku zote za majaribio yangu na imani yangu Kocha ataona uwezo wangu na ikiwezekana nisajiliwe Simba.”

“Kama nikipata nafasi ya kucheza katika uwanja mzuri nitaweza kuonyesha uwezo wangu zaidi ya sasa kwa sababu nimekuja Tanzania kwa nia ya kuichezea Simba, hivyo nitapambana kuwaridhisha wenyeji wangu,” alisema Sekuhawa.

Mzambia huyo atakayekuwa nchini kwa wiki mbili kufanya majaribio katika kikosi hicho amewahi kunolewa na George Lwandamina wa Yanga walipokuwa pamoja katika klabu ya Zesco.

 

Liuzio ampamba

Straika wa Simba Juma Liuzio ambaye amekuwa na nafasi finyu ya kucheza mara kwa mara katika kikosi hicho msimu huu, aliwashtua mabosi wake wa Msimbazi

kwa kuwaambia wasimuache Sakuhawa kwani bonge la mchezaji.

Liuzio amewahi kucheza pamoja na Mzambia huyo Zesco United, alisema Sekuhawa ni mchezaji mzuri na uzoefu wake utaisaidia Simba kimataifa.

Simba mwakani itarejea kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya kimataifa tangu mwaka 2013 iliposhiriki Ligi ya Mabingwa na kung’olewa mapema na Recreativo do Libolo ya Angola. Itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

“Sakuhawa tulicheza naye Zesco na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2016 kabla ya kutolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, hivyo sio

mchezaji wa kumbeza ingawa sijamuona tangu nilipoondoka Zambia,” alisema.

Simba ndiyo inayoongoza Ligi Kuu mpaka sasa ikiwa na pointi 23. Ligi hiyo imesimama kupicha Chalenji.