Mwili wa Mzee Majuto watolewa Hospitali ya Muhimbili

Dar es Salaam. Wasanii mbalimbali, ndugu jamaa na marafiki wamejitokeza katika hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya shughuli za mazishi ya mwigizaji Amri Athumani 'Mzee Majuto'.

Wengi wapo nje ya jengo la kuhifadhia maiti wakisubiri mwili huo utolewe unatarajiwa kwenda kusaliwa msikiti wa Maamur.

Tayari gari maalum la msikiti huo litakalotumika kumbeba limewasili hapa huku taratibu nyingine za kumuandaa zikiendelea.

Awali Rais wa shirikisho la filamu Tanzania, Simon Mwakifamba amesema, Mzee Majuto ataagwa saa nane mchana katika viwanja vya Kamrijee na saa kumi Jioni atasafirishwa kwenda nyumbani kwake Tanga kwa mazishi.

“Taarifa hii tumewasiliana na familia nikwamba, Mzee Majuto ndugu jamaa na marafiki watatoa heshima za mwisho na baada ya hapo mwili utaelpelekwa nyumbani kwake Tanga kwa ajili ya mazishi” amesema Simon Mwakifamba

Mtoto wa Mzee Majuto, Ashrafu amesema ratiba kamili ya mwili wa Mzee Majuto ni kwamba asubuhi  mwili utaoshwa katika Hospitali ya  Muhimbili na shughuri zote ndogo ndogo zitafanyika hapo na baada ya hapo mwili utapelekwa kiwanja cha Karimjee kwa ajili ya kuagwa saa nane mchana,na saa kumi mwili utasafirishwa Tanga kwa ajili ya kuzikwa"