Mwanariadha kumaliza hasira zake madola

Muktasari:

Mashindano ya Jumuia ya Madola yatafanyika mwakani nchini Austrialia

Arusha: Mwanariadha Gabriel Geay baada ya kushindwa kushiriki mashindano ya Dunia yaliyofanyika London mwaka huu ameanza kujifua kwa ajili ya mashindano ya madola mwakani.

Geay alishinda hata kuanza mbio hizo kutokana na maumivu ya goti lililokuwa likimsumbua tangu akiwa kambini Arusha, lakini alikwenda kibishi London ili kuitetea Taifa lake kwenye michuano hiyo, kabla ya kunyanyua mikono juu sambamba na Magdalena Shauri aliyeishia njiani kwenye mbio ndefu.

 “Nilipofika London kabla ya mashindano tulifanyiwa vipimo wanariadha wote ndipo daktari akanishauri nisisumbuke kushiriki mashindano yale kwa kuwa tatizo langu lilikuwa kubwa na endapo ningeshiriki historia yangu ya riadha ndio ilikuwa inaishia hapo,” alisema Geay.

 Mara baada ya kurudi nchini mwanariadha huyo aliendelea kuufuta ushauri wa Daktari wa kutofanya mazoezi yoyote ili apate muda mzuri wa kuupumzisha mwili wake kwa miezi kadhaa kabla ya kuanza mazoezi mepesi.

 “Kwa muda wote nilikuwa nyumbani na mara chache nilikuwa nakwenda kumwona daktari kujua maendeleo ya mguu wangu na sasa namshukuru Mungu naendelea vizuri na tayari nimeanza mazoezi mepesi”

Mwanariadha huyo wa mbio za 5,000 Mita amejumuishwa kwenye timu ya taifa ya riadha itakayopiga kambi Lushoto kujiandaa na michuano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika Aprili mwakani nchini Australia.