Mwadui FC yabeba zigo la Ndanda kubaki Ligi Kuu

Mwanza. Matumaini ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao kwa Klabu ya Ndanda itajulikana kesho Jumatano iwapo itashinda mchezo wake dhidi ya Mwadui, mpambano utakaopigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Ndanda ambao wamekusanya pointi 23 wapo nafasi ya 15, ambapo wanapaswa kushinda mechi hiyo ili kuishusha Majimaji wenye alama 24 katika nafasi ya 14 ili kufufua matumaini ya kubaki Ligi Kuu.

Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Ndanda, Malale Hamsini ameapa kuwa mchezo huo hawataki sare wala kupoteza kwani una ushindani kwao pekee na si kwa wapinzani wao.

Alisema kuwa hakuna mchezaji mwenye tatizo lolote anayeweza kukosa mpambano huo, isipokuwa ni maamuzi yake kuamua amtumie nani na amuache nani.

“Mechi yetu hii ni ya kushinda tu,hatutaki sare wala kupoteza,tunajua Mwadui hawana presha kwakuwa wameshajihakikishia kubaki Ligi Kuu hivyo ni ushindani umebaki kwetu na ninashukuru vijana wangu wote wapo fiti,” alisema Hamsini.

Kocha huyo aliongeza kuwa kikubwa ni wadau na wapenzi wa Soka mkoani Mtwara kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu hiyo ili kupata hamasa zaidi na kufikia melengo.

Naye Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu alisema kuwa mkakati wao ni kushinda mechi zilizobaki ili kumaliza Ligi vizuri na kwenye nafasi nzuri.

“Tutakwenda kusaka pointi tatu,hatujali cha kwamba hatushuki au la,huu ni mpira na malengo yetu ni kushinda na niseme kwamba wapinzani wetu wasitegemee mteremko,”alisema Bizimungu.