Mvua ya mabao yaanza Kanda ya Ziwa

JUZI kikosi cha Stand United kilijitupa uwanjani kwa mara ya kwanza kujipima nguvu dhidi ya Wapinzani wao wa Jadi Mwadui FC na kujikuta ikiambulia kipigo cha mabao 2-0,lakini Kocha wake Amars Niyongabo amesema kuwa hiyo haimuumizi kichwa.

 

Katika mchezo huo ambao ulipigwa kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga kila timu ilionyesha uwezo wake,lakini ‘Chama la Wana’ ikajikuta katika wakati mgumu na kukubali kibano hicho.

 

Kocha Niyongabo alisema kuwa licha ya kupoteza mpambano huo hiyo haimpi shida kwani lengo lake lilikuwa ni kubaini wapi kuna mapungufu,jambo ambalo alifanikisha.

 

Niyongabo raia wa Burundi alisema kuwa katika mchezo huo alibaini kuwepo kwa udhaifu mdogo kwenye eneo la mabeki kutokuwa makini,hivyo katika mechi nne alizopanga kucheza atayafanyia kazi.

 

“Kupoteza siyo ishu,kikubwa nilichotaka ni kuona ni wapi kuna mapungufu,ambapo nimebaini mabeki wangu kutokuwa makini kwahiyo kwenye mechi nne nilizopanga kucheza kabla ya Ligi vijana wataimarika”alisema Niyongabo.

 

Kwa upande wake Kocha wa Mwadui,Ally Bizimungu alisema kuwa kwa sasa anapambana vikali kuunda kombinesheni kali ambayo itafanya maangamizi pindi Ligi Kuu itakapoanza.

 

“Nashukuru kuona vijana wangu wanaendelea kufanya vizuri ninachotaka ni kupata kombinesheni hatari kwa ajili ya Ligi,naamini timu itakuwa bora zaidi ya hapa”alitamba Bizimungu.

 

Katika mtanange huo,Atu Joseph (Ghana) na Edwine Edwine raia wa Nigeria ndio walitakata kwa kila mmoja kufunga bao moja moja na kuifanya timu yao ya Mwadui kutoka uwanjani kwa shangwe.