Muuaji wa Brazil atua Friends Rangers

DAR ES SALAAM. Mtanzania pekee aliyeifunga timu ya taifa ya Brazil, Jabir Aziz 'Stima' amesema kwa sasa atapumzika kucheza Ligi Kuu Bara msimu huu, badala yake anageukia Ligi Daraja la Kwanza kuisaidia Friends Rangers.

Aziz Stima aliifunga Brazil katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika Dar es Salaam mwaka 2010 na Taifa Stars kuchapwa 5-1.

Stima anasema lengo la kutua Friends Rangers ni kuipa sapoti timu hiyo, akiamini huduma yake kwa kushirikiana na wenzake waone kama watafanikiwa kuipandisha kucheza Ligi Kuu msimu wa 2019/20

"Kama kuna timu imeweza kuwaibua mastaa wengi wanaotamba katika Ligi Kuu basi ni Friends Rangers na ndio maana nimeamua kujiunga nao, ili kuisaidia kama Mungu atasaidia iweze kupanda na yenyewe.

"Tupo wachezaji wengi tuliotoka ligi kuu na nia yetu ni kujitolea kikamilifu kwa ajili ya Friends Rangers, kwani ni timu yenye mchango mkubwa katika maisha yetu ya soka,"anasema.

Stima amewahi kuzichezea timu mbalimbali ikiwemo Azam FC, JKT Ruvu kwa sasa inajulikana kama JKT Tanzania, Mwadui FC na Ndanda FC ya Mtwara.