Mubenga: Ommy Dimpoz amepotea kimuziki

Thursday September 7 2017

 

By FRANK NGOBILE

Dar es Salaam. Meneja wa zamani wa Ommy Dimpoz, Mubenga amekiri mwanamuziki huyo kwa sasa anashuka kimuziki tofauti na mwanzo na badala yake kinachomfanya kusikika ni kiki mbalimbali na si muziki tena.

Akizungumza na MCL Digital, Mubenga anasema kwa miaka sita amekuwa pamoja na Ommy na kumsaidia kutegeneza muziki mzuri uliomfanya kuwa juu tofauti na sasa ambavyo anazungumziwa kwa migogoro baadhi na wasanii wenzake kama Diamond Platnumz.

“Tangu niachane na Ommy Dimpoz mnaona kabisa hayupo tena kwenye chati za muziki, stori utazomsikia kwa sasa ni kama hivyo migogoro ya hapa na pale ambapo kipindi changu haikuwa hivyo na hiyo inaonesha wazi kwamba badala ya kupanda zaidi ameanza kushuka.”

Aidha Mubenga alipoulizwa kuhusu mambo anayoyakumbuka kutoka kwa Ommy Dimpoz kwa kipindi hichi alisema hakuna kitu anachokikumbuka kwa msanii huyo na wala hajawahi kumkumbuka.

“Simkumbuki kwa chochote na wala sijawahi kumkumbuka sababu kwanza sina mawasiliano naye hivyo kila mmoja yuko mbali na upeo wa mwenzake,” aliongeza.

Kwa sasa Mubenga anasimamia wasanii wengine chini ya kampuni yake ya Bengaz Ent.